array(0) { } Radio Maisha | Watu 3 wauliwa Njoro, familia 400 zaachwa bila makao

Watu 3 wauliwa Njoro, familia 400 zaachwa bila makao

Watu 3 wauliwa Njoro, familia 400 zaachwa bila makao

Zaidi ya familia mia nne zimeachwa bila makao eneo la Sigaon Mau Mashariki kufuatia mapigano baina ya jamii mbili. Mapigano hayo yaliyoanza jana jioni yamesababisha watu watatu kuaga dunia na wengine zaidi ya kumi kujeruhiwa. Mkuu wa Polisi eneo la Molo, Benard Muinde hata hivyo amesema usalama umeimarishwa japo hakuna aliyekamatwa kuhusu kisa hicho.

Aidha zaidi ya shule kumi zimefungwa. Shule ambazo zimeathirika ni pamoja na Sigaon Academy, ile ya upili ya na msingi ya Ogiek, Shule ya Msingi ya Tiritagoi na ile ya upili ya Nessuit miongoni mwa nyingine.

Hayo yakijiri, Inspekta Mkuu wa Polisi, Joseph Boinnet ameagiza uchunguzi kufanywa kuhusu kuuliwa kwa watu watatu akiwamo afisa wa polisi katika mji wa Kenyenye Kaunti ya Kisii. Boinett amesema yeyote atakayepatikana na mauaji hayo atachukuliwa hatua kali za kisheria. Afisa wa polisi Tom Onyango, Hesbon Onkoma na Paul Onderi waliuliwa na umati wa watu katika kituo cha kuegesha magari mjini humo.

Mvutano baina ya umma na maafisa wa polisi ulianza baada ya wakazi kuandamana hadi kituo cha polisi kulalamikia kuuliwa kwa muhudumu mmoja wa magari eneo hilo.

Mili ya waliouliwa imepelekwa katika Hifadhi ya Kisii Level Five ikisubiri kufanyiwa upasuaji. Wakazi mjini Kisii wamewalaumu polisi kwa mauaji hayo.