array(0) { } Radio Maisha | Obado akana kuhusika katika mauaji ya Sharon Otieno

Obado akana kuhusika katika mauaji ya Sharon Otieno

Obado akana kuhusika katika mauaji ya Sharon Otieno

Gavana wa Migori, Okoth Obado amejitokeza hadharani leo hii kwa mara ya kwanza kukana kuhusika katika mauaji ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo, Sharon Otieno. Akiwahutubia wanahabari jijini Nairobi akiwa ameandamana na mkewe, wanawe wawili na maafisa wengine wa Kaunti ya Migori, Obado amesema kwamba kuhusishwa na kisa hicho kumeisababishia mahangaiko makuu familia yake.

Obado ametoa wito kwa maafisa wa usalama wanaochunguza mauaji ya Sharon kuharakisha uchunguzi ili wahusika wakuu wakabiliwe kwa mujibu wa sheria.  

Wakati uo huo gavana huyo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kumwombea katika kipindi hiki kigumu ambapo anakabiliwa na tuhuma nzito.

Hayo yanajiri huku mahakama ikiagiza mshukiwa mkuu wa mauaji ya Sharon, Michael Oyamo azuiliwe kwa siku 14 zaidi huku uchunguzi kuhusu kifo hicho ukiendelea. Jaji Luka Kimaru ameitikia wito wa upande wa mashtaka kwamba kuna masuala mengi yanayostahili kupewa muda katika uchunguzi huo kukiwamo kuchunguza mawasiliano ya Oyamo na washukiwa wengine wanaolengwa.