array(0) { } Radio Maisha | Michael Oyamo kufikishwa mahakamani leo

Michael Oyamo kufikishwa mahakamani leo

Michael Oyamo kufikishwa mahakamani leo

Mshukiwa Mkuu wa mauaji ya Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo Sharon Otieno, Michael Oyamo atafikishwa katika mahakama ya Nairobi Jumatano. Oyamo ambaye alikamatwa muda mfupi baada ya kuachiliwa alisafirishwa hadi hapa jijini Nairobi jana jioni. Kulingana na Polisi Oyamo atashtakiwa hapa jijini ili kumhakikishia usalama wake, hasa baada ya wakazi wa Homa Bay kuapa kumwadhibu.

Hapo Jana Gavana wa Migori Okoth Obado ambaye pia amehusishwa pakubwa na mauaji hayo alihojiwa kwa zaidi ya saa nane na maafisa wa upelelezi mjini Kisumu. Kulingana na Ripoti za maafisa wa polisi ni kwamba Obado alitakiwa kuelezea kuhusu uhusiano wake na Sharon, iwapo alimfahamu na iwapo anahusika kwa vyovyote na mimba aliyokuwa akiibeba Sharon. Aidha inaarifiwa kuwa alikubali kufanyiwa uchunguzi wa DNA ili kubainisha ukweli, vile vile kukiri kumfahamu Sharon japo hakuelezea kwa kina uhusiano baina yao ulikuwa wa aina gani. Cliff Ombeta ni Wakili wa Obabo.

Polisi aidha walimtaka Obado kuelezea mara ya mwisho alizungumza na Sharon vile vile mwanahabari wa Shirika la Nation Barack Oduor na Oyamo. Taarifa ya Obado italinganishwa na ile wachunguzi watakayoipata kutoka kwa mawasialino ya simu baina ya watatu hao, ambayo yanaendelea kutathiminiwa. Gavana huyo anasemekana kukana kuhusika kwa vyovyote na mauaji ya Sharon.

Hata hivyo polisi wanasema kwamba hawakumaliza kumhoji Obado huku upelelezi ukitarajiwa kuendelea leo hii, japo haijabainika utafanyikia eneo lipi, kwani Gavana aliondoka Kisumu jana jioni punde baada ya kuhojiwa.

Kuhusu usalama wa Gavana huyo, Ombeta amesema kuwa hawana hofu.

Ikumbukwe Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi DCI George Kinoti alisema kwamba gavana huyo aliachiliwa baada ya kuahidi kuwa atashirikiana kikamilifu katika uchunguzi huo.

Hayo yanajiri huku washukiwa wengine wanne wa maujai hayo wakiwa wanatafutwa, huku gari lililotumika kumsafirisha Sharon likiwa halijulikani liliko. Polisi wanasema huenda iko hapa jiji Niarobi au katika taifa jirani la Tanzania.