array(0) { } Radio Maisha | Obado azuiliwa na maafisa

Obado azuiliwa na maafisa

Obado azuiliwa na maafisa

Baada ya shinikizo tele za kukamatwa na kuhojiwa kufuatia kisa cha kuuliwa kikatili kwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo, Sharon Otieno, hatimaye leo Gavana wa Migori, Okoth Obado amerekodi taarifa. Obado amehojiwa na Idara ya Upelelezi, DCI katika makao yake makuu jijini Kisumu kuhusu kifo cha mwanafunzi huyo anayedaiwa kwamba alikuwa katika uhusiano wa kimapenzi naye.

Obado alihojiwa kwa zaidi ya saa nne baada ya kuagizwa kufika katika ofisi za DCI kutokana na kutajwa kwake pakubwa kuhusu mauaji hayo. Baada ya hayo, aliondolewa akiwa ndani ya gari la maafisa wa polisi huku ikisemekana kuwa alielekezwa katika uwanja wa ndege ili kufikishwa jijini Nairobi.

Haya yakijiri, hatma ya mshukiwa mkuu wa mauaji ya Sharon Otieno Mchieal Oyamo ya kufikishwa mahakamani haijulikani baada ya Kituo cha Polisi cha Homa Bay kumwachilia kabla ya kukamatwa tena muda mfupi baadaye na maafisa wa upelelezi DCI. Sasa inaarifiwa kuwa mshukiwa huyo atafikishwa katika Mahakama ya Milimani hapa jijini Nairobi wala si Mahakama ya Homa Bay ilivyokuwa ikitarajiwa.

Kamanda wa Kaunti ya Homa Bay, Marius Tum amesema walimwachilia mshukiwa huyo ambaye alikuwa afisa wa KDF kufuatia agizo la Jaji wa Mahakama ya Homa Bay, Lester Simiyu ambalo lilitaka idara ya poilisi kumwasilisha kufikia leo saa tatu la sivyo wamwachilie huru.

Jana, Jaji Simuyu alikataa kuipa idara ya polisi siku kumi zaidi za kuendelea kumzulia Oyamo huku wakifanya uchunguzi na kuwapa saa ishirini na nne ambazo zilikamilika leo saa tatu asubuhi wakati maafisa hao wa upelelezi walipomkamata.

Aidha mwanahabari, Barrack Oduor ambaye aliwakwepa waliomteka nyara yeye na Sharoni, alifikia katika ofisi hizo kujibu maswali na kurekodi taarifa yake. Oduor ambaye alikuwa jijini Nairobi, alitakiwa kujiwasilisha katika ofisi hizo vilevile akiwa amebeba nguo alizokuwa amevalia wakati wa kisa hicho.

Mwili wa Sharon ulipatikana katika Msitu wa K'odero siku ya Jumanne wiki iliyoipita ukiwa na majera ya kudungwa kisu mara nane mbali na kubakwa.