array(0) { } Radio Maisha | Magoha awaonya wanaolenga kushiriki udanganyifu katika mitihani ya kitaifa

Magoha awaonya wanaolenga kushiriki udanganyifu katika mitihani ya kitaifa

Magoha awaonya wanaolenga kushiriki udanganyifu katika mitihani ya kitaifa

 

''Vituo vya mitihani vitakavyoshiriki udanganyifu katika mitihani ya kitaifa vitafungwa na wasimamizi wake kuchukuliwa hatua kali. '' Kauli hiyo imetolewa na  Waziri wa Elimu, Amina Mohammed baada ya mkutano na washikadau mbalimbali wa elimu kuelezea hatua zilizopigwa kufikia sasa katika matayarisho ya mitihani hiyo.

 Amina aidha amesema wizara hiyo inashirikiana na idara mbalimbali za serikali kuhakikisha mitihani inalindwa. Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Mitihani, KNEC George Magoha kwa upande wake amesisitiza suala la kuwawajibika kikamilifu watakaoshiriki udanganyifu katika mitihani hiyo

Magoha aidha amewasihi watahiniwa kujiepusha kuhadaiwa kupitia mitihani bandia ambayo inasambazwa na kuwataka kuzingatia zaidi waliyofunzwa katika silabasi wanapojoitayarisha kwa mitihani hiyo. Ili kuzuia udanganyifu wakati wa mitihani hiyo, KNEC itawatuma wasimamizi wa mitihani waliosajiliwa na Tume ya Huduma za Walimu, TSC ili iwe rahisi kuwafuatilia. Amesema awali baadhi ya waliosimamia mitihani hawakuwa walimu waliosajiliwa na TSC.

Kila mtahiniwa ataketi umbali wa mita 1.2 kutoka kwa mwenzake ili kuepusha udanganyifu. Aidha KNEC imenunua makontena 415 yatakayotumiwa kuhifadhi mitihani huku kila kituo cha mtihani kikiwa na maafisa wawili wa usalama. Aidha, kwenye maeneo ya mijini baada ya mitihani, kipindi kisichozidi dakika 30 kinastahili kutumiwa kuzirejesha karatasi za mitihani katika makontena ili kuhifadhiwa.

Mitihani ya Kitaifa ya Darasa la Nane, K.C.P.E itang'oa nanga Oktoba 30 huku ile ya kidato cha nne, K.C.S.E iking'oa nanga Novemba 2.