array(0) { } Radio Maisha | Naibu Jaji Mkuu, Philomena Mwilu apata afueni mahakamani

Naibu Jaji Mkuu, Philomena Mwilu apata afueni mahakamani

Naibu Jaji Mkuu, Philomena Mwilu apata afueni mahakamani

Kesi dhidi ya Naibu Jaji Mkuu, Philomena Mwilu katika Mahakama ya Milimani imesitishwa kuambatana na agizo la Mahakama Kuu. Hakimu Lawrence Mugambi ametoa uamuzi huo baada ya kupokezwa maagizo sahihi kutoka kwa Jaji Chacha Mwita wa Mahakama Kuu baada ya kurekebisha dosari zilizokuwapo katika agizo la kwanza.

 Hakimu Mugambi hata hivyo amesema kikao kingine kitaandaliwa Oktoba 22 wakati mahakama itakapofahamishwa kuhusu yaliyoafikiwa katika Mahakama Kuu ambapo Jaji Mwilu amewasilisha kesi kupinga kushtakiwa kwake katika mahakama ya hadhi ya chini vilevile kuishtaki ofisi ya DPP na ile ya DCI kwa misingi ya kulenga kumdhalilisha.

Hakimu Mugambi aidha ameratibu tarehe 5 Septemba kuwa siku ambayo atatoa uamuzi kuhusu ombi la mshtakiwa wa pili, Stanley Muluvi la kusitishwa kwa kesi dhidi yake katika mahakama hiyo kuambatana na agizo la Mahakama Kuu ambalo limetolewa leo hii.

Awali  upande wa mashtaka uliwasilisha ujumbe wa Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma, DPP kwamba anahakikisha haki za washukiwa zinalindwa. Ujumbe huo uliwasilishwa kupitia wakili wa upande wa mashtaka, Dorcas Oduor.

Ikumbukwe mawakili wa Mwilu wamelalamika kwamba mteja wao alidhalilishwa kwa kukamatwa na kuwasilishwa katika mahakama ya hadhi ya chini huku wakidai huenda kuna njama ya kumbandua ofisini.

Kando na hayo, upande wa mashtaka ulitaka ufafanunuzi kuhusu namna vikao vingeendeshwa ikizingatiwa upande wa utetezi una mawakili takriban 44 wanaowajumuisha maseneta na wabunge mawakili hali ambayo huenda ikachangia vikao kuchukua muda mrefu iwapo wote watapewa nafasi ya kuwasilisha hoja zao.

Miongoni mwa tuhuma zinazomkabili Mwilu ni utumiaji mbaya wa mamlaka, ukwepaji ulipaji kodi, ufisadi, ukiukaji wa sheria. anashtumiwa kwa kutumia mbinu za kilaghai kupata fedha zinazodaiwa zilikuwa za Benki ya Emperial iliyo chini ya mrasimu, vilevile alizawidiwa fedha ili kupendelea katika uamuzi wa kesi, suala linaloenda kinyume na maadili ya idara ya mahakama.