array(0) { } Radio Maisha | Chama cha Third Way Alliance chapendekeza kushtakiwa kwa waliokuwa makamishna wa IEBC

Chama cha Third Way Alliance chapendekeza kushtakiwa kwa waliokuwa makamishna wa IEBC

Chama cha Third Way Alliance chapendekeza kushtakiwa kwa waliokuwa makamishna wa IEBC

Chama cha Third Way Alliance kimependekeza kushtakiwa kwa waliokuwa makamishna wa IEBC, Connie Maina na Margaret Mwachanya kwa kutaka kurejea katika tume hiyo baada ya kujiuzulu.

Kiongozi wa chama hicho, Ekuru Aukot amesema ni kinaya kwa wawili hao kushinikiza kurejea ilhali walipoondoka, walilalamikia uongozi duni wa Mwenyekiti, Wafula Chebukati.

Aidha amesema wawili hao hawastahili kuruhusiwa kushikilia wadhifa mwingine wa umma kwa kuwa wamedhihirisha kutowajibika kazini. Chama hicho kimesema huenda hatua ya makamishna hao imechochewa kisiasa.

Mbali na hayo, chama hicho kimependekeza kuvunjwa kwa jopokazi lililobuniwa kufanikisha uwiano nchini kufuatia ushirikiano baina ya Rais Uhuru na Raila Odinga huku kikimpa Rais Kenyatta makataa ya siku saba kulivunja jopo hilo. Kimesema jopo hilo halikubuniwa kisheria kwa kuwa umma haukuhusishwa katika kutoa maoni.
 
Aidha kimesema utakuwa utumiaji mbaya wa rasilmali za umma kwa jopo hilo kuendelea kuhudumu kwani linatumia fedha za umma kuendeleza shughuli zake. Vilevile kimesema majukumu ya jopo hilo yanalingana na yanayotekelezwa na taasisi nyingine za serikali mfano Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa, NCIC, hivyo haina umuhimu. Hata hivyo, chama hicho kimeeleza kuunga mkono ushirikiano kati ya Uhuru na Raila.