array(0) { } Radio Maisha | Rais Uhuru Kenyatta ameshuhudia kutiwa sahini kwa makubaliano mawili

Rais Uhuru Kenyatta ameshuhudia kutiwa sahini kwa makubaliano mawili

Rais Uhuru Kenyatta ameshuhudia kutiwa sahini kwa makubaliano mawili

Rais Uhuru Kenyatta ameshuhudia kutiwa sahini kwa makubaliano mawili ambayo yatafanikisha uwekezaji wa kampuni mbili za Marekani  kima cha zaidi ya shilingi bilioni 20, humu nchini.

Kampuni za Kipeto Wind Energy na Twiga Foods zinatarajiwa kuanza kutoa huduma zake nchini Kenya huku zikijikita katika sekta ya uzalishaji nguvu za umeme na uwepo wa chakula mtawalia.

Uhuru ambaye alikutana na mwenyeji wake wa Marekani Donald Trump katika Ikulu ya White House ameelezea kuridhishwa kwake na mkutano baina yake na Trump ambapo masuala mbalimbali likiwemo suala tata la ugaidi lilijadiliwa kwa kina pamoja na upanuzi wa biashara kati ya Kenya na Marekani.

Aidha, suala la upanuzi wa barabara inayoziunganisha miji ya Nairobi na Mombasa ilijadiliwa kwa kina pamoja na miradi ingine ya maendeleo inayolihusisha bara Afrika kwa jumla ilijadiliwa.

Ikumbukwe kuwa katika siku za hivi karibuni, Kenya imekuwa mshirika mkubwa wa kibiashara na Uchina japo ziara ya Uhuru nchini Marekani imedhihirisha utayarifu wa Kenya kuwakubali washirika wote kibiashara.

Baadaye wiki hii, Uhuru ambaye amekuwa rais wa pili barani Afrika kualikwa katika Ikulu ya White House baada ya mwenzake wa Nigeria Muhammadu Buhari, anatarajia kumpokea Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May ambaye atazuru Kenya kabla ya kuelekea jijini Beijing, Uchina kuhudhuria mkutano wa pamoja wa bara Afrika na Uchina.