array(0) { } Radio Maisha | Raia wa kigeni walio nchini kinyume na sheria kufurushwa

Raia wa kigeni walio nchini kinyume na sheria kufurushwa

Raia wa kigeni walio nchini kinyume na sheria kufurushwa

Idadi kubwa ya visa vya utovu wa usalama vinavyoripotiwa nchini, hutekelezwa na raia wa kigeni wanaoishi nchini kinyume na sheria.

Waziri wa Masuala ya Ndani ya Nchi Fred Matiang'i amesema wizara yake imebainisha kuwa visa vya mauaji, ulanguzi wa dawa za kulevya na biashara haramu hutekelezwa na raia hao. Kufuatia hali hiyo amewaagiza maafisa wa usalama wakiongozwa na Makamishna wa kaunti kufanya msako na kuwafurusha nchini raia hao, iwapo hawana stakabadhi zinazohitajika.

Amesema msako dhidi ya raia hao utaanza usiku wa leo, katika maeneo ya Eastlands Nairobi.

Kulingana na Matiangi, wengi wao hudanganya kuwa katika ndoa ili kuendelea kuishi humu nchini. Amesema msako huo, utajumuisha kuhakikisha walio katika ndoa wana vyeti vinavyohitajika, huku akisema wale ambao ndoa yao imedumu kwa kipindi cha chini ya miaka mitatu sharti wawe na vibali vya kufanya kazi nchini.

Kando na hayo Waziri huyo amesema kuna Wakenya wanaozuiliwa katika magereza ya mataifa ya nje, kwa tuhuma za ulanguzi wa dawa za kulevya baada ya kulaghaiwa.

Amesema wametia saini mkataba wa utendakazi na Idara ya Uhamiaji kuhusu suala hilo, akisema kufikia sasa raia sitini waliopatikana wakiishi humu nchini kinyume na sheria wamerejeshwa kwao. Aidha maafisa ishirini na wanane wa idara ya uhamiaji waliohusishwa na ufisadi wamefutwa kazi.

Matiangi alikuwa akizungumza wakati wa mkutano uliowaleta pamoja makamishna wa kaunti zote 47 na makamanda wa polisi, uliofanyika jijini Nairobi