array(0) { } Radio Maisha | TSC yaitikia kilio cha walimu

TSC yaitikia kilio cha walimu

TSC yaitikia kilio cha walimu

Kwa mara nyingine, serikali imeitikia kilio cha walimu huku Tume ya Huduma za Walimu, TSC ikikubadili kuzitathmini upya sera kuhusu utendakazi wao. Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo, Nancy Macharia amemwagiza Mkurugenzi wa Kutathmini Viwango vya Elimu, Reuben Nthamburi kuandaa kikao cha dharura na walimu wakuu wa shule za msingi na wale wa upili kujadili suala hilo.

Katika hotuba ya Macharia iliyosomwa kwa niaba yake na mwakilishi wake, Rita Wahome wakati wa kukamilika kwa kongamano la kila mwaka la walimu wakuu wa shule za msingi jijini Mombasa, amewaagiza wakurugenzi wa TSC kufanya vikao na walimu wakuu wa shule za msingi na upili kuhusu suala la marekebisho ya sera za elimu kwa kipindi cha wiki mbili zijazo.

Macharia amesema hatua hiyo inalenga kuondoa dukuduku kuzihusu baadhi ya sera ambazo zimekuwa zikiibua mijadala miongoni mwa washikadau wa elimu ili kuhakikisha kuna mazingira bora ya kufanyia kazi kwa walimu hao na hatimaye kufaninisha azimio la kuimarisha viwango vya elimu nchini.

Agizo hilo linajiri siku moja baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuagiza kurekebishwa kwa baadhi ya sera za elimu, ikiwamo ile ya uhamisho wa walimu wakuu ambayo imekuwa ikitekelezwa na TSC. 

Sasa inasubiriwa kuona iwapo Chama cha Kitaifa cha Walimu, KNUT kitaendeleza vitisho vya kuitisha mgomo Septemba Mosi ikizingatiwa kwamba hilo ni mojawapo la masuala yaliyokuwa yakishinikizwa na chama hicho.

Zaidi ya walimu wakuu elfu kumi walihudhiria kongamano hilo lililoanza rasmi Jumatatu wiki hii.