array(0) { } Radio Maisha | Mwenyekiti wa NLC, Mohhamed Swazuri akamatwa

Mwenyekiti wa NLC, Mohhamed Swazuri akamatwa

Mwenyekiti wa NLC, Mohhamed Swazuri akamatwa

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi EACC Khalake Waqo, amesisitiza kwamba maafisa saba wakuu wa serikali ambao wamekamatwa mapema leo watazuiliwa katika makao makuu ya Tume hiyo hadi Jumatatu watakapofikishwa mahakamani kujibu mashtaka dhidi yao. Akizungumza muda mfupi uliopita, Waqo amesema wanafuata taratibu zote za kisheria katika kuwachukulia hatua washukiwa wakuu wa sakata mbalimbali za ufisadi.

Amesema wanashirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma DPP kikamilifu katika vita dhidi ya ufisadi. Waqo aidha amesema wameandaa misururu ya mikutano na DPP Noordin Haji kuhusu sakata mablimbali za ufisadi hasa zinazowahusu maafisa wakuu serikaini.

Maafisa ambao wamekamatwa ni Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi Mohammed Swazuri, Naibu Mwenyekiti Abigael Mbagaya na Afisa Mkuu Mtendaji wa NLC  Aziz Chavangi. Wengine ni Meneja Mkurugenzi wa Shirika la Reli Atanas Maina, Salome Munubi, Francis Karimi Mugo, Gladys Mwikali na Obadiah Mbugua Wainaina.

Awali waziri wa zamani Chirau Ali Mwakwere ambaye alifika katika makao makuu ya EACC alisema alitaka kufahamu kinachoendelea kufuatia hatua hiyo ya maafisa hao kukamatwa.

Ikumbukwe Haji aliidhinisha kukamatwa kwa Swazuri na wenzake kufuatia sakata ya ufisadi wakati wa kuwafidia walioathirika kufuatia mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa SGR. Inaarifiwa jumla ya shilingi bilioni nne zilifujwa wakati wa mpango huo. Aidha ripoti ya ukaguzi ilionesha baadhi ya watu ambao hawakuathirika na ujanzi huo walifidiwa na wengine kulipwa zaidi ya mara moja.