array(0) { } Radio Maisha | Yaliyojiri mwaka mmoja baada ya uchaguzi mkuu

Yaliyojiri mwaka mmoja baada ya uchaguzi mkuu

Yaliyojiri mwaka mmoja baada ya uchaguzi mkuu

Mwaka mmoja tangu kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu, mengi yamejiri nchini. Ilianza tukio la kihistoria la  kubatilishwa kwa ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta na Mahakama ya Juu chini ya uskani wa Jaji Mkuu, David  Maraga.

Ni uamuzi ulioibua mseto wa hisia na hatimaye kuwalazimu Wakenya kurejea debeni Oktoba 26. Uchaguzi huo nao ukakumbwa na visanga vyake ambapo Kinara Mkuu wa Muungano wa NASA, Raila Odinga akaamua kuususia uchaguzi huo hatua iliyopunguza ushindani na kumfanya Rais Uhuru Kenyatta kutwaa awamu nyingine ya uongozi.

Aidha maandalizi ya marudio hayo yalishamiri vituko kutoka Tume ya Uchaguzi, IEBC na kwa wakati mmoja Mwenyekiti wa tume hiyo, Wafula Chebukati kuonekana kuwa tayari kujiuzulu iwapo wanasiasa wasingesitisha miingilio ya kisiasa.

Haya hivyo hakujiuzulu na badala yake aliyekuwa mmoja wa makamishna wa IEBC, Roselyne Akombe akafungua ukurasa wa kujiuzulu kwa makamishna wa tume hiyo akidai tume haikuwa tayari kwa marudio ya uchaguzi vilevile kutokuwa na imani na usimamizi wa Chebukati katika kuandaa uchaguzi huru na wa haki vilevile kumtaka aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji, Ezra Chiloba ajiuzulu wadhifa wake.

Licha ya hayo yote, marudio ya uchaguzi yalifanyika huku Rais Uhuru Kenyatta akiibuka mshindi na hatimaye kutangaza ajenda nne kuu anazolenga kutekeleza katika awamu yake ya mwisho ya uongozi. Ajenda hizo ni afya kwa wote, utoshelezo wa chakula, ujenzi wa makazi zaidi yatakayokodishwa kwa bei nafuu na kuimarishwa kwa sekta ya viwanda ili kubuni nafasi zaidi za ajira.

Hata hivyo upinzani haukusitisha mbwembwe zake baada ya kuapishwa kwa Rais Kenyatta. Muungano wa NASA ukaamua vilevile kuandaa hafla ya  kumwapisha kinara wake, Raila Odinga, halfa iliyofanyika katika Bustani ya Uhuru na kuongozwa na Mwanaharakati Miguna Miguna na Mbunge wa Ruaraka, TJ Kanjwang. Hafla hiyo ikawa mwanzo wa kusambaratika kwa NASA kwani Raila aliachwa pekee ajiapishe huku vinara wenza, Kalonzo Musyoka, Musalia Muadavadi na Moses Wetangula wakisusia hafla hiyo.

Aidha ukawa ndiyo mwanzo wa masaibu ya Miguna Miguna ambaye alianza kuandamwa na serikali kwa misingi ya kuwa mwanachama wa kundi haramu la National Resistance Movement , NRM lililotangaza kususiwa kwa bidhaa za kampuni kadhaa zikiwamo Safaricom, Brookside na Bidco. Hatimaye akafurushwa nchini kwa misingi kwamba si raia wa Kenya na hadi sasa hajarejea.

Hatua aliyochukua Raila Machi 9 ya kuamua kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta kupitia Handshake, bila shaka ilibadili mkondo wa siasa za humu nchini. Wengi waliitaja hatua hiyo kuwa mwamko mpya kwa taifa na itakayoleta umoja huku wengine wakiitaja kuwa usaliti mkubwa kwa vinara wenza wa Raila ikizingatiwa hawakuwapo wakati wa Handshake. Tangu hatua hiyo ya kihistoria, muungano wa NASA umeonekana kuyumbayumba huku kila mwamba ngoma akivutia kwake. Wabunge wanaomuunga mkono Raila ambao awali walijaza kejeli dhidi ya serikali ya Uhuru, sasa wameonekana kulegeza misimamo.

Hata hivyo viongozi wanaomuunga mkono Naibu wa Rais, William Ruto wamesikika wakiushtumu uhusiano mpya kati ya Uhuru na Raila wakisema huenda ni njama ya kuzima ndoto ya Ruto kuwania urais mwaka 2022. Licha ya mbwembwe hizo, Uhuru na Ruto wamekazana kwamba huu si wakati wa siasa ila wa kuwahudumia Wakenya.

Ikiwa imesalia miaka minne kabla ya kuandaliwa kwa uchaguzi mwingine, kibarua kilichoko sasa ni uteuzi wa makamishna wengine wa Tume ya Uchaguzi, IEBC baada ya kujiuzulu kwa  Paul Kurgat, Margaret Mwachanya,  Connie Maina, na Roseylne Akombe hali ambayo imeifanya tume hiyo kusalia na idadi ya makamishna ambayo haitoshi kuendeleza shughuli za tume. Kulingana na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Adan Duale, mchakato wa uteuzi wa makamishna wapya utaanza kwa kipindi cha mwezi mmoja ujao.

Aidha kibarua kingine ambacho kimesalia ni kwa mahakama kukamilisha kesi mbalimbali zilizotokana na uchaguzi mkuu. Tayari maamuzi mbalimbali yamefanywa ambapo uchaguzi wa wengine umedumishwa na mahakama huku chaguzi nyingine zikibatilishwa japo waathiriwa wamekata rufaa wakisubiri hatma ya mwisho.