array(0) { } Radio Maisha | Serem ahojiwa kwa wadhifa wa ubalozi

Serem ahojiwa kwa wadhifa wa ubalozi

Serem ahojiwa kwa wadhifa wa ubalozi

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kuratibu Mishahara ya Wafanyakazi wa Umma, SRC Sarah Serem amekana madai kwamba alikuwa na nia mbaya dhidi ya wabunge alipoidhinisha kupunguzwa kwa mishahara yao. Serem ameyasema hayo mbele ya Kamati  ya Ulinzi na  Masuala ya Kigeni katika Bunge la Kitaifa ambayo imewahoji watu walioteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kuwa mabalozi katika mataifa mbalimbali.

Serem ambaye amekuwa wa kwanza kuhojiwa na kamati hiyo leo asubuhi, amesema si mishahara ya wabunge pekee iliyopunguzwa ila pia ya maafisa wengine wa umma lakini wabunge ndiyo waliolalamika zaidi kwa kuwa walikuwa na njia za kuwasilisha ghadhabu yao. Serem ameomba radhi kwa wasioridhishwa na maamuzi mbalimbali aliyofanya akihudumu katika SRC japo amesema maamuzi aliyofanya yalikuwa ya manufaa kwa wananchi na yalifanywa kwa ushirikiano wa makamishna wenza.

Aidha baadhi ya wabunge wamemtaja Serem kuwa mtu mwenye udikteta na asiyeeleweka vyema suala ambalo Serem amelipuuza. Serem ambaye ameteuliwa kuhudumu katika wadhifa wa ubalozi nchini Uchina ameahidi kuiwakilisha Kenya vyema endapo ataidhinishwa na bunge.  

Aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha  Upelelezi, DCI Ndegwa Muhoro ambaye ameteuliwa kuwa balozi wa Kenya nchini Malasyia aidha amehojiwa huku akitakiwa kujieleza kutokana na madai kwamba akihudumu katika kitengo cha upelelezi alikuwa akisambaratisha uchunguzi wa kesi mbalimbali. Aidha madai ya kufanikisha mauaji ya kiholela na kujihusisha katika uuzaji wa ardhi kwa njia za ulaghai  yameibuliwa dhidi yake huku mkenya mmoja akiwasilisha waraka kwa kamati hiyo kutomwidhinisha kwa misingi hiyo.

Aliyekuwa Msemaji wa Ikulu, Manoah Esipisu amesema atatumia wadhifa wa ubalozi kuimarisha biashara kati ya Kenya na Uingereza. Amesema Uingereza ina kampuni nyingi ambazo zinaweza kutumiwa kuimarisha ushirikiano huo.

Mwingine aliyehojiwa ni aliyekuwa Kamanda wa Jeshi la Wanahewa, Samuel Thuita ambaye ameteuliwa kuwa balozi wa Kenya nchini Israel. Thuita ametakiwa kueleza namna atakavyohakikisha ajenda nne kuu za serikali zinaafikiwa kupitia uhusiano kati ya Kenya na Israel. Wengine watachujwa siku ya Ijumaa kabla ya kamati hiyo kuwasilisha ripoti yake bungeni