Balala ashtumiwa vikali na wataalam wa mifugo

Balala ashtumiwa vikali na wataalam wa mifugo

Muungano wa Wataalam wa Mifugo umemshtumu vikali Waziri wa Utalii, Najib Balala kwa kuwalimbikizia lawama madaktari wa mifugo kutokana na vifo vya vifaru 10 katika Bunga ya Tsavo. Wataalam hao wamemtaka Balala kuwarejesha kazini mara moja madaktari waliosimamishwa kazi kutokana na kisa hicho.

Katika kikao na wanahabari jijini Nairobi, Mwenyekiti wa Muungano wa  Wataalam wa Mifugo, Benson Kibore amemtaka Balala kuwarejesha kazini mara moja madakari aliyowasimamisha kazi akisema hawapaswi kulaumiwa kutokana na vifo vya wanyama hao kwani walitekeleza jukumu lao kwa ukamilifu.

Muungano huo aidha umesema  anayestahili kuwajibikia vifo vya vifaru hao ni aliyetoa agizo la kuhamishwa kwao kutoka Mbuga ya Nakuru. Muungano huo umemtaka Waziri Balala kutoa taarifa za kina kuhusu kuhamishwa kwa vifaru hao ilhali inaelekea kwamba mazingira ambayo walihamishiwa hayakuwa salama.

Vifaru takriban 10 walikufa kwa kipindi cha wiki mbili katika Mbuga ya Tsavo baada ya kuhamishwa kutoka ile ya Nakuru huku ripoti ya awali ikionesha kwamba walikufa kutokana na unywaji wa maji yenye chumzi nyingi. Siku ya Jumanne, Balala aliomba radhi kutokana na matamshi yake ya 'They Can go to Hell' dhidi ya wanaomlaumu kutokana na vifo vya wanyama hao.