array(0) { } Radio Maisha | Gavana wa Laikipia apata ushindi mahakamani

Gavana wa Laikipia apata ushindi mahakamani

Gavana wa Laikipia apata ushindi mahakamani

Mahakama mbalimbali nchini zimefanya maamuzi katika kesi za uchaguzi mkuu uliopita ambapo ushindi wa Gavana wa Laikipia, Nderitu Muriithi umedumishwa sawa na ule wa Mbunge wa Mbeere Kusini, Geoffrey Kingang'i. Aidha Mahakama ya Rufaa imebatilisha uamuzi wa Mahakam Kuu ambayo ilitulia mbali ushindi wa Mbunge wa Gatundu Kusini, Ann Wanjiku Kibe. Majaji watatu waliofanya uamuzi katika kesi hiyo wamesema kuwa makosa yaliyoshuhudiwa wakati wa uchaguzi hayakutosha kufutilia mbali usindi wa Kibe.

Mpigakura kwa jina Sammy Ndung'u amepata pigo mahakamani baada ya Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali kesi aliyowasilisha kupinga ushindi wa Gavana wa Laikipia, Nderitu Muriithi huku mahakama ikimwagiza kulipa kima cha shilingi milioni 1 ambayo ni gharama ya kesi. Majaji Asike Makhandia, Fatuma Sichale na Sankale Ole Kantai waliofanya uamuzi katika kesi hiyo wamesema haikuwa na msingi thabiti wa kutosha kubatilisha ushindi wa Gavana Muriithi. Mpiga-kura huyo alidai kwamba uchaguzi huo haukundaliwa kwenye baadhi ya maeneo kufuatia vurugu za kijamiii.

Kwingineko mahakama imetupilia mbali kesi iliyokuwa ikipinga ushindi wa Mbunge wa Mbeere Kusini, Geoffrey Kingang'i. Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani na Kamau Nyutu kwa madai kwamba King'angi alitumia ushirikina kushinda kiti hicho.

Shahidi wa mlalamishi, Kevin Murimi aliiambia mahakama kwamba Kingang'i alifanya matambiko mwezi mmoja kabla ya uchaguzi kwa kuchinja ng'ombe usiku, akisaidiwa na waganga wawili.

Kadhalika alidai kwamba Kingang'i  aliwahonga wapiga-kura. Hata hivyo mahakama imesema madai hayo hayakuthibitishwa  mahakamani.