array(0) { } Radio Maisha | Ushindi wa Seneta wa Lamu wabatilishwa na mahakama

Ushindi wa Seneta wa Lamu wabatilishwa na mahakama

Ushindi wa Seneta wa Lamu wabatilishwa na mahakama

Seneta wa Lamu ambaye ni wa Chama cha Jubilee, Anwar Loitiptip amevuliwa wadhifa huo na Mahakama ya Rufaa ya Mombasa ambayo imebatilisha uamuzi wa Mahakama Kuu iliyodumisha ushindi wake. Uamuzi huo umetolewa kufuatia rufaa  iliyowasilishwa na  mpinzani wake Hassan Albeity aliyewania wadhifa huo kwa tiketi ya Chama cha Wiper huku mahakama ikiiagiza Tume  ya Uchaguzi, IEBC kuandaa uchaguzi mdogo kwenye kaunti hiyo kumchagua seneta mpya. Majaji Alnashir Visram, Wanjiru Karanja na Martha Koome wametoa uamuzi katika kesi hiyo wakisema uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu. Jamaa wa Albeity wameleezea furaha yao kutokana na uamuzi huo wa mahakama.

Mnamo Februari 9, Jaji wa Mahakama Kuu Asenath Ongeri aliitupilia mbali kesi iliyowasilishwa na Albeity kwa misingi kwamba haikuwasilishwa kwa wakati ufaao.

Huku Seneta Loitiptip akipata pigo mahakamani, Mbunge wa Marakwet Mashariki, Kangongo Bowen anaendelea kusherehekea uamuzi wa Mahakama ya Rufaa mjini Eldoret ambayo imedumisha ushindi wake. Akitoa uamuzi huo, Jaji Erastus Githinji ameukosoa uamuzi wa Mahakama Kuu iliyotupilia mbali ushindi wa mbunge huyo akisema  ushahidi uliowasilishwa katika kesi hiyo haukutosha kubatilisha ushindi wake.

Awali, Jaji wa Mahakama Kuu, George Kimondo alifutiliwa mbali ushindi wa Bowen kwa misingi ya udanganyifu na kutumiwa kwa vituo viwili kujumlisha kura za uchaguli licha ya kwamba havikuwa vimechapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali. Mbunge huyo ameelezea kuridhishwa na uamuzi huo wa mahakama.

Hayo yanajiri huku Mahakama ya Rufaa ikidumisha ushindi wa Mbunge wa Turkana Mashariki, Mohammed Lokir, uamuzi huo ulitolewa na Jaji Erastus Githinji na Hannah Okwengu. Wawili hao wamesema ushahidi uliowasilishwa na aliyekuwa  Mbunge, Nicholas Ngikor haukutosha kuonesha kwamba uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu.