array(0) { } Radio Maisha | Mahakama yadumisha ushindi wa Mbunge wa Nandi Hills Alfred Keter

Mahakama yadumisha ushindi wa Mbunge wa Nandi Hills Alfred Keter

Mahakama yadumisha ushindi wa Mbunge wa Nandi Hills Alfred Keter

Mbunge wa Nandi Hills, Alfred Keter amepata afueni baada ya Mahakama ya Rufaa kudumisha ushindi wake wakati wa uchaguzi mkuu uliopita. Wakitoa uamuzi huo, majaji Erastus Githinji, Fatuma Sichale na Anna Okwengu wamesema Keter alichaguliwa kwa njia halali, hivyo kutupilia mbali uamuzi wa awali wa Mahakama Kuu uliofutilia mbali ushindi wake mnamo mwezi Machi mwaka huu. Jaji Kimondo alifutilia mbali ushindi huo kwa madai ya kuwapo visa vya udanganyifu na kwamba haukuandaliwa kwa njia huru na haki.

Hata hivyo, majaji hao wamesema mlalamishi, Bernard Kitur hakuwasilisha ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa mbunge huyo aliendesha kampeni baada ya kukamilika kwa muda uliowekwa na Tume ya Uchaguzi IEBC. Akiwahutubia wafuasi wake muda mfupi baada ya uamuzi huo kutolewa, Keter anasema masaibu yake yalichangiwa na hatua yake ya kupaaza sauti kuhusu masuala ya ufisadi, hasa visa vinavyowahusisha viongozi mbalimbali.

Amesisitiza kwamba hakufanya kosa lolote na kwamba ataendelea kuwatetea wanyonge katika jamii ambao wanaendelea kuathiriwa na ufisadi. Amesikitishwa na hasara wanayopata wakulima kwenye Kaunti za Elgeyo Marakwet, Uasin Gishu na Nandi, kutokana na suala la baadhi ya watu kunufaika na fedha ambazo wangelipwa kwa mazao yao ya kilimo. 

Keter amesema hababaishwi na yeyote na kwamba ataendeleza juhudi zake za kupigania haki za Wakenya ili kutokomeza jinamizi la ufisadi. Ikumbukwe IEBC ilimtangaza Keter kuwa mshindi wakati wa uchaguzi mkuu uliopita kwa kupata kura elfu 28, 923 dhidi ya kura elfu 13, 872 alizopata Bernard Kitur. Awali kesi hiyo ilikuwa imewasilishwa na Robert Kemei ambaye alijiondoa.