array(0) { } Radio Maisha | Wakazi wa Kisumu wajitayarisha kwa ziara ya Obama

Wakazi wa Kisumu wajitayarisha kwa ziara ya Obama

Wakazi wa Kisumu wajitayarisha kwa ziara ya Obama

Aliyekuwa Rais wa Marekani, Barack Obama anatarajiwa kuwasili nchini siku ya Jumatatu wiki ijayo huku serikali ya Kauti ya Kisumu ikijiandaa vilivyo kwa ziara ya kiongozi huyo ambaye ataizuru kaunti hiyo kabla ya kuelekea nyumbani kwa nyanyaye eneo la Kogelo, Kaunti ya Siaya.

Wenyeji wa Kaunti ya Kisumu watakuwa na fursa ya kipekee kufuatilia ziara hiyo baada ya serikali ya kaunti hiyo kujiandaa kupeperusha ziara hiyo moja kwa moja kutoka Kaunti ya Siaya hadi Bustani ya Jomo Kenyatta ambapo wenyeji watakuwa wakitizama.

Kwa mujibu wa afisa Mkuu wa Utalii na Mawasiliano kwenye Kaunti ya Kisumu, Achie Alai, hatua hiyo ni ya kuhakikisha kuwa wenyeji wanahisi kuhusishwa kikamilifu katika ziara hiyo.

Ndege itakayombeba Obama itatua katika Uwanja wa Kimataifa wa Kisumu siku ya Jumatatu na kushiriki mazungumzo mafupi na Gavana Anyang’ Nyong’o kabla ya kuelekea Kogello, Kaunti Siaya. Achie hata hivyo amesisitiza kuwa ziara ya Obama ni ya kifamilia, hivyo serikali haitajihusisha pakubwa.

Tayari vyombo vya habari vya kimataifa vimeanza kupiga kambi kwenye Kaunti za Kisumu na Siaya kufuatilia ziara hiyo ya kwanza ya Obama nchini tangu astaafu, baada ya kuiongoza Marekani kwa mihula miwili. Naibu Gavana wa kaunti hiyo, Mathew Owili ameeleza matumaini kwamba ziara hiyo itakuwa ya manufaa kwa wakazi wa Kisumu na kuwataka wafanyabiashara eneo hilo kuchukua fursa hiyo kujiendeleza.

Owili aidha ameeleza umuhimu wa ziara hiyo wakati huu ambapo viongozi wa serikali na wa upinzani wameahidi kushirikiana kwa ajili ya umoja wa kitaifa.Inatarajiwa kwamba Obama tafanya kikao na Rais Uhuru Kenyatta vilevile Kinara wa Chama cha ODM, Raila Odinga atakapowasili kabla ya kuelekea Kisumu.