array(0) { } Radio Maisha | Washukiwa wa mkasa wa Bwawa la Solai waachiliwa kwa dhamana

Washukiwa wa mkasa wa Bwawa la Solai waachiliwa kwa dhamana

Washukiwa wa mkasa wa Bwawa la Solai waachiliwa kwa dhamana

 

Mahakama imelikubali ombi la kuwaachilia kwa dhamana washukiwa tisa wa mkasa wa Bwawa la Solai uliosababisha vifo vya watu arubaini na wanane. Tisa hao wamechiliwa Mahakama ya Naivasha kwa dhamana ya shilingi laki tano na mdhamini wa kiasi sawa na hicho au pesa taslimu shilingi milioni 2.5. Licha ya pingamizi la upande wa mashtaka kwamba tisa hao huenda wakawatatiza mashahidi wa serikali, Hakimu Mkuu wa mahakama hiyo Joseph Karanja aliagiza waachiliwe.

Vilevile aliwaagiza washukiwa kuwasilisha stakabadhi zao za usafiri mahakamani na kujiwasilisha katika Ofisi ya Idara ya Upelelezi DCI mjini Nakuru kila baada ya wiki mbili. Tisa hao akiwamo mmiliki wa bwawa hilo Perry Mansukh na Meneja wa Kampuni ya Patel Coffee Estates, Vinoj Kumar, wamekuwa wakizuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Naivasha.

Haya yanajiri wakati afisa mmoja mkuu wa serikali Julius Kavita ambaye alikuwa ameshtakiwa kwa makosa 48 ya kuua bila kukusudia akiondolewa mashtaka na afisa mwingine wa ngazi za chini katika serikali ya Kaunti ya Nakuru Luka Kipyegen akichukua nafasi hiyo na kushtakiwa. Kipyegen ni Naibu Kamishna wa eneo la Rongai. Hatua hiyo ilizua hisia kinzani kutoka kwa mawakili wa utetezi.

Wakili Lawrence Kariuki ambaye anamwakilisha Kipyegen alishangazwa na hatua ya Mkuu wa Mashtaka ya Umma DPP, Noordin Haji kuagiza kukamatwa kwa Kavita na baadaye jina lake kuondolewa. Mahakama imetenga tarehe 3 mwezi ujao kuwa siku ya kuanza kusikilizwa wa kesi hiyo.