array(0) { } Radio Maisha | KUPPET yapewa makataa ya wiki mbili kumuomba msamaha mwathiriwa wa Moi Girls

KUPPET yapewa makataa ya wiki mbili kumuomba msamaha mwathiriwa wa Moi Girls

KUPPET yapewa makataa ya wiki mbili kumuomba msamaha mwathiriwa wa Moi Girls

Chama cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kadri, KUPPET kimepewa makataa ya siku kumi na nne kuomba msamaha kwa familia ya msichana wa Shule ya Wasichana ya Moi jijini Nairobi baada ya kutoa ripoti kuwa mwanafunzi huyo hakubakwa ila wasichana wenzake ndio waliotaka kumwadhibu baada ya kukataa kushiriki ngono ya jinsia moja. Makataa hayo yametolewa na wanaharakati wa masuala ya wanawake katika kikao na wanahabari jijini Nairobi.

Mwakilishi Wadi wa Laini Saba, Cecilia Achieng' aliyeongoza kikao hicho ameitaka Idara ya Upelelezi kufanya uchunguzi kikamilifu kuwachukulia hatua wahusika. Aidha, ameitaka KUPPET iweke wazi mbinu walizotumia kufanya uchunguzi huo, na ni nani aliyeidhinisha uchunguzi wao.

Mwakilishi wa familia ya mwanafunzi huyo, Sheikh Yusuf Nasur amesema familia imesikitishwa na ripoti hiyo na kutaka KUPPET iheshimu familia ya mwanafunzi huyo.

Aidha, Sheikh Yusuf amesema familia ya mwanafunzi huyo ililazimika kuhamia makao mapya wakidai kutishiwa maisha na watu wasiojulikana.

Mmoja wa wanaharakati hao, MaryLize Biubwa ambaye pia aliwahi kudhulumiwa kimapenzi anasema ripoti hiyo ya KUPPET inakiuka maadili ya jamii kwa kusema hakubakwa ila aliadhibiwa tu na wanafunzi wenzake.

Siku ya Alhamisi wiki hii, Chama cha Mawakili wa Kike, FIDA kilitaka viongozi wa KUPPET wachunguzwe kwa madai ya kupanga kutatiza uchunguzi wa kisa hicho.

Vilevile Mwanaharakati wa kisiasa, Brian Weke alipinga vikali ripoti hiyo akisema si mara ya kwanza kwa madai ya usagaji kuripotiwa shuleni, na kwamba kisa hicho kiliporipotiwa, walikuwapo mashahidi ambao walimzungumzia mwanamume mmoja aliyeonekana katika shule hiyo, na kwamba hakuna aliyezungumzia suala la usagaji.

Ikumbukwe kisa hicho kilichotokea tarehe 2 mwezi uliopita kilisababaisha kuvunjwa na kubuniwa upya kwa bodi ya shule na mwalimu mkuu kujiuzulu. Uchunguzi wa polisi wa kumtambua aliyehusika unakaribia kukamilika, huku ukaguzi wa sampuli za chembechembe za DNA za wanaume thelathini na wawili na zile zilizokusanywa kutoka kwa mwathiriwa ukiendelea katika maabara ya serikali.