array(0) { } Radio Maisha | Gavana Ojaamong awachiliwa kwa dhamana

Gavana Ojaamong awachiliwa kwa dhamana

Gavana Ojaamong awachiliwa kwa dhamana

Gavana wa Busia, Sospepter Ojaamong amepata afueni baada ya Mahakama ya Milimani kumwachilia huru kwa dhamana pamoja na washukiwa wengine watatu baada ya kukaa korokoroni kwa kipindi cha siku mbili. Wanne hao wakiwamo Benard Yaite, Allan Ekweny na Samuel Ombui wanaohudumu katika nyadhifa mbalimbali kwenye serikali ya Kaunti ya Busia wameachiliwa huru kwa dhamana ya shilingi milioni tatu au mdhamini ya shilingi milioni mbili ama dhamana ya shilingi milioni moja pesa taslimu kila mmoja. 

Akitoa uamuzi huo Jaji, Douglas Ogoti aidha amewaagiza washtakiwa kupiga ripoti katika ofisi za Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi, EACC kila Ijumaa ya mwisho ya mwezi hadi kesi dhidi yao itakaposikilizwa tena. 

Walipofikishwa mahakamani mapema wiki hii, wanne hao walikana mashtaka ya utumiaji mbaya wa mamlaka, hali iliyochangia kupotea kwa kati ya shilingi milioni 8 na milioni 20 za Kaunti ya Busia. Mahakama aidha imetoa agizo la kukamatwa kwa washukiwa wengine wanne ambao hawajajisalimisha kwa polisi hadi sasa.

Mahakama imetoa uamuzi wa kuwaachilia washukiwa hao kwa dhamana baada ya kupinga sababu zilizotolewa na upande wa mashtaka kwamba huenda wakatatiza ushahidi iwapo wataachiliwa huru, ikisema sababu za kutosha hazijatolewa kuonesha namna watakavyohitilafiana na mashahidi.

Awali baadhi ya wabunge wa eneo la Busia walimtembelea Ojamong katika Jumba la Integrity alikokuwa akizuiliwa kabla ya kufikishwa mahakamani.Gavana Ojaamong amekuwa wa kwanza miongoni mwa magavana wanaohudumu kukesha kizuizini huku viongozi wengine kadhaa wakiwamo magavana wa zamani na wa sasa vilevile mawaziri wakitarajiwa kufunguliwa mashtaka.