array(0) { } Radio Maisha | FIDA yadai walimu wanapanga kutatiza uchunguzi wa kisa cha kubakwa kwa mwanafunzi wa shule ya Moi, Nairobi

FIDA yadai walimu wanapanga kutatiza uchunguzi wa kisa cha kubakwa kwa mwanafunzi wa shule ya Moi, Nairobi

FIDA yadai walimu wanapanga kutatiza uchunguzi wa kisa cha kubakwa kwa mwanafunzi wa shule ya Moi, Nairobi

Siku moja baada ya Chama cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo KUPPET kutoa ripoti iliyochapishwa katika gazeti moja humu nchini, na kuonesha kwamba huenda mwanafunzi anayedaiwa kubakwa katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Moi, Nairobi alidhulumiwa na wanafunzi wenzake bwenini, Chama cha Mawakili wanawake FIDA kinataka walimu wa shule pamoja na KUPPET wachunguzwe kwa madai ya kupanga kutatiza uchunguzi dhidi ya kisa hicho.

Ikumbukwe kisa hicho kilichotokea tarehe 2 Juni mwaka huu kilisbabaisha kuvunjwa na kubuniwa upya kwa bodi ya shule na mwalimu mkuu kujiuzulu. Uchunguzi wa polisi wa kumtambua aliyehusika na kisa hicho unakaribi kukamilika, huku ukaguzi wa sampuli za chembechembe za DNA za wanaume thelathini na wawili na zile zilizokusanywa kutoka kwa mwathiriwa ukiendelea katika maabara ya serikali.

Hayo yakijiri, Mwanaharakati wa kisiasa Brian Weeke na Mwakilishi wa eneo la Kibera Laini Saba Cecilia Ayot wameghadhabishwa na KUPPET, huku Mweke akisema si mara ya kwanza kwa madai ya usagaji kuripotiwa shuleni. Amesema kwamba kisa hicho kiliporipotiwa, walikuwapo mashahidi ambao walimsema mwanamume mmoja alionekana katika shule hiyo, na kwamba hakuna aliyezungumzia suala la usagaji. Ameitaja ripoti ya KUPPET kuwa isiyo na msingi na inayolenga kuwalinda walimu. Kwa upande wake Ayot amesema watatumia idara zilizopo kuhakikisha KUPPET inawajibishwa dhidi ya ripoti hiyo.