array(0) { } Radio Maisha | Wabunge wataka Waziri Rotich abanduliwe

Wabunge wataka Waziri Rotich abanduliwe

Wabunge wataka Waziri Rotich abanduliwe

Rais Uhuru Kenyatta ana makataa ya hadi siku ya Ijumaa wiki hii kumsimamisha kazi Waziri wa Fedha, Henry Rotich kwa kutozuia uagizaji wa sukari kimagendo na ambayo si salama kwa matumizi ya binadamu. Makataa hayo yametolewa na kundi la wabunge wa eneo la Magharibi ya Nchi.

Wakizungumza katika majengo ya bunge, wabunge hao wamesema iwapo Rais Kenyatta hatachukua hatua hiyo, huenda wakalazimika kuwasilisha bungeni mswada wa kutokuwa na imani na Waziri Rotich.Ikumbukwe mwezi Agosti mwaka uliopita, Waziri Rotich alichapisha notisi ya kuwaruhusu wafanyabiashara mbalimbali kuagiza sukari. Wabunge hao aidha wamemshtumu Rotich kwa madai ya kuzembea kazini na kutowajibikia utendakazi wake.

Hayo yakijiri, Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa Nchini, KEBs limefichua kwamba ni kampuni nne pekee ambazo ziliruhusiwa na shirika hilo kuagiza sukari ghafi. Miongoni mwa kampuni hizo ni West Kenya na Kampuni ya Menengai. Shirika hilo limeyasema hayo mbele ya kamati ya pamoja ya kilimo na biashara ya Bunge la Kitaifa, ambayo inachunguza madai ya kuingizwa nchini kwa sukari kimagendo na ambayo si salama kwa matumizi ya binadamu.

Wabunge aidha wametaka ufafanuzi kuhusu namna wananchi wanavyoweza kuitambua sukari ghafi na iliyo tayari kwa matumizi, suala ambalo KEBs imesema si rahisi kwa mwananchi kutambua.

Huku kamati hiyo ikitarajiwa kukamilisha vikao vyake leo hii na kuandaa ripoti, mvutano umeshuhudiwa miongoni mwa wanakamati hiyo kuhusu idadi ya maswali ambayo kila mbunge anastahili kuuliza, hali ambayo imeibua majibizano kati yao na Mwenyekiti, Kanini Kega. Kamati hiyo aidha inatarajiwa kuwahoji mawaziri, Henry Rotich, Ceciliy Kariuki na Mwangi Kiunjuri.