Rais Kenyatta ayaagiza mashirika yote ya umma kuchapisha taarifa kuhusu tenda

Rais Kenyatta ayaagiza mashirika yote ya umma kuchapisha taarifa kuhusu tenda

Ili kudumisha uwazi katika idara zinazohusika na ununuzi wa bidhaa serikalini, Rais Uhuru Kenyatta ameyaagiza mashirika yote ya umma kuchapisha taarifa zote kuhusu tenda mbalimbali zinazotolewa kuanzia tarehe moja mwezi wa Julai mwaka huu.

Katika taarifa kupitia Msemaji wa Ikulu, Rais Kenyatta amesema kuchapishwa kwa tenda hizo kutatoa fursa kwa umma kutathmini namna huduma za serikali zinavyoendeshwa ili kudumisha uwazi na kukabili ufisadi.

Miongoni mwa taarifa zitakazochapishwa ni kiwango cha fedha kilichotumiwa kununulia bidha mbalimbali na waliopewa tenda za kuwasilisha bidhaa hizo.

Aidha kuanzia mwezi Januari mwaka 2019, bidhaa zote zinazonunuliwa na serikali zitanunuliwa kupitia mfumo wa kidigitali wa IFMIS.

Waziri wa Masuala ya Ndani ya Nchi, Fred Matiang'i ameagizwa kuhakikisha mfumo huo ni salama na hauingiliwi, ili kuepusha kutumiwa kwake kuendeleza ufisadi. Maafisa wote wa ununuzi watawajibishwa katika utendakazi wao na watahitajika kuwajibikia rasilimali za umma wanazozisimamia.