Abiria wote waliokuwa katika ndege iliyoanguka Jumanne, waliaga

Abiria wote waliokuwa katika ndege iliyoanguka Jumanne, waliaga

Abiria wote waliokuwa katika ndege iliyohusika katika ajali Jumanne usiku kwenye Msitu wa Aberdare walifariki dunia. Mwenyekiti wa kampuni ya ndege ya Fly SAX iliyohusika ajali hiyo Charles Wako amethibitisha taarifa hizo huku akituma rambirambi kwa familia za walioaga.

Tangazo hilo limetolewa muda mfupi uliopita wakati shughuli ya kuwatafuta manusura ikiendelea.
Mapema leo Katibu wa Wizara ya Uchukuzi, Paul Maringa alisema mabaki ya ndege hiyo yalipatikana Kusini Magharabi ya msitu huo eneo la Njambini, Kaunti ya Nyandarua.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya Fly Sax alisisitiza kuwa ndege hiyo ilikuwa katika hali nzuri kabla ya kusafiri, kadhalika kuendeshwa na marubani wenye tajriba.

Wakati uo huo, Rais Uhuru Kenyatta ametuma risala za rambirambi  kwa familia za abiria wanane na marubani wawili waliofariki dunia kutokana na ajali ya ndege katika Msitu wa Aberdare eneo la Njambini. Rais Kenyatta ameahidi kutoa usaidizi utakaohitajika kufuatia mkasa huo.

 Aidha amevishukuru vikosi vyote vilivyoendeleza oparesheni ya kuisaka ndege hiyo vikiwamo Shirika la Msalama Mwekundu, Mamlaka ya Safari za Angani, Shirikla la Huduma za Wanyamapori, KWS na jeshi la wanahewa.

 Ndege hiyo ilitoweka siku ya Jumanne ilipokuwa safarini kutoka Kitale kuja katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta.