Kaunti zimeboresha mifugo kwa kuwawezesha wakulima milioni 1.1 kupata njia za kisayansi za kuzalisha mifugo wao.

Kaunti zimeboresha mifugo kwa kuwawezesha wakulima milioni 1.1 kupata njia za kisayansi za kuzalisha mifugo wao.

Utalii wa ndani kwa ndani umeimarika kwa asilimia 37.3 ukilinganishwa na wa mwaka jana kufuatia juhudi za serikali za kaunti kuwaelimisha wananchi kuhusu maeneo mbalimbali ya kutalii. Ripoti kuhusu suala hili imesomwa na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana, Josephat Nanok, alipolihutubia taifa kuhusu yaliyoafikiwa katika kufanikisha ugatuzi.

Nanok amesema suala zima la ugatuzi limepiga hatua na kubadili maisha ya wananchi kukiwamo kufanikishwa kwa miradi mbalimbali ya maendeleo. Vilevile, ameangazia ushirikiano baina ya baraza hilo na idara nyingine katika kuafikia malengo yake kwani mwaka uliopita, ndilo lililokuwa suala kuu.

Katika juhudi za kupunguza gharama serikali za kaunti zimepunguza marupurupu ya wawakilishi wadi kwa asilimia 67.

Akizungumzia kilimo Nanok amesema Serikali za Kaunti zimeboresha mifugo kwa kuwawezesha wakulima milioni 1.1 kupata njia za kisayansi za kuzalisha mifugo wao.

Vilevile amesema serikali za kaunti zimeweka juhudi za kuboresha sekta ya afya kwa kuhakikisha watoto walio chini ya miaka mitano wanapata chanjo. Kufikia sasa, asilimia 70 ya watoto wamepata chanjo.

Katika kikao cha mwaka uliopita, aliyekuwa Mwenyekiti, Peter Munya alilalamikia kucheleweshwa kwa mgao wa fedha kutoka serikali ya kitaifa, kuhangaishwa na maseneta kadhalika migomo kadhaa ya wahudumu wa afya.

Hata hivyo, hali imebadilika mwaka huu huku magavana na maseneta wameonekana kuwa na uhusiano bora zaidi kadhalika serikali kuu kuendelea kusisitiza utayarifu wake kuziwezesha serikali za kaunti.

Akizungumzia hali ya anga, Nanok ametoa wito kwa Bunge la Kitaifa kupitisha pendekezo la fedha za kukabila majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya anga. Pendekezo hilo likipitishwa asilimia mbili ya fedha kutoka serikali ya kitaifa zitatengewa Baraza la Kitaifa la Mabadiliko ya Anga.

Vilevile Nanok ametoa wito kwa serikali ya kitaifa kufadhili elimu ya watoto wachanga ECDE akisema sekta hiyo imeimarika marudufu. Kufikia sasa, kuna takriban shule elfu ishirini na tano, mia moja thelathini na tatu za ECDE za umma.

Nanok amesema misururu ya visa vya ufisadi vimepunguza imani ya wananchi kwa miradi yote inayoendelezwa na serikali za kaunti na kuitaka mahakama kuwachukulia hatua wote watakaopatikana na makosa ya wizi wa fedha hizo.

Kwa mujibu wa Waziri wa Ugatuzi, Eugene Wamalwa, baadhi ya sheria za ugatuzi zinafanyiwa marekesbisho ikiwamo ile ya  uhusiano baina ya serikali ya kitaifa na za kaunti ya mwaka 2012. Kadhalika, sheria za kaunti zinatarajiwa kufanyiwa mabadiliko ili kuwapa manaibu gavana, majukumu rasmi. Vilevile huenda likabuniwa baraza la serikali za kaunti.

Kufikia sasa serikali za kaunti zimepokea jumla ya shilingi trilioni 1.