makatibu wote katika wizara, mashirika na idara mbalimbali za serikali wameagizwa kujiondoa ofisini mara moja

makatibu wote katika wizara, mashirika na idara mbalimbali za serikali wameagizwa kujiondoa ofisini mara moja

Tangazo la Rais Uhuru Kenyatta kwamba serikali yake haitawavumilia tena watu fisadi serikalini, limeanza kuzitikisa idara mbalimbali za serikali. Siku mbili tu baada ya Rais kuagiza wakaguliwe upya, makatibu wote katika wizara, mashirika na idara mbalimbali za serikali wameagizwa kujiondoa ofisini mara moja, kupisha ukaguzi, ili wale wasiofaa waachishwe kazi. Mkuu wa Utumishi wa Umma, Francis Kinyua ametangaza mwongozo kuhusu ukaguzi huo, kwa lengo la kukabili ufisadi.

Katika waraka huo, wakuu wote wa ununuzi na uhasibu katika wizara na mashirika yote ya serikali, wameamriwa kujiuzulu mara moja. Kabla ya kujiondoa, wameagizwa kuwaachia manaibu wao majukumu waliyokuwa wakitekeleza. Mbali na hayo, kila mmoja ametakiwa kuwasilisha maelezo ya binafsi katika ofisa ya Mkuu wa Utumishi wa Umma, katika Jengo la Harambee jijini Nairobi, kabla ya tarehe 8 Juni, yaani Ijumaa wiki hii. Maelezo hayo yanahusu mali wanayomiliki, ithibati ya umiliki wa mali hizo na walikohudumu kabla ya ajira serikalini. Waraka huo aidha umebainisha kwamba licha ya hatua hii kulenga kuhakikisha kuwa maafisa wanaofaa pekee wanasalia ofisini na kurejesha imani ya Wakenya, shughuli hiyo itaendeshwa kwa uwazi kwa mujibu wa katiba, bila kukiukwa kwa haki za yeyote. Msisitizo katika waraka huo aidha ni kuhusu kujitolea kwa Rais Uhuru Kenyatta kuhakikisha kuwa idara ya utumishi wa umma inawahudumia Wakenya ipasavyo, bila yeyote kutumia nafasi yake kujinufaisha.

Hatua hii imejiri siku mbili tu baada ya agizo la Rais Uhuru Kenyatta, wakati wa maadhimisho ya Madaraka, Kaunti ya Meru.