Kamati ya Bunge ya Haki na Masuala ya sheria imekutana na Tume ya Uchaguzi IEBC ili kufahamu jinsi tume hiyo inavyoendesha majukumu yake

Kamati ya Bunge ya Haki na Masuala ya sheria imekutana na Tume ya Uchaguzi IEBC ili kufahamu jinsi tume hiyo inavyoendesha majukumu yake

Kamati ya Bunge ya Haki na Masuala ya sheria imekutana na Tume ya Uchaguzi IEBC ili kufahamu jinsi tume hiyo inavyoendesha majukumu yake ikizingatiwa tayari makamishna wanne walijiuzulu, na tume hiyo kusaliwa na watatu pekee; Wafula Chebukati, Abdi Guliye na Boya Molu. Mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati amewaongoza makamishna katika kikao hicho, na kusema kwamba shughuli za tume zinaendelea kawaida, lakini hawawezi kuandaa mikutano ya pamoja ikizingatiwa idadi ya makamishna waliosalia. 

Aidha amesema wanaendeleza shughuli ya kuyahamisha makao makuu ya IEBC kutoka katika jumba la Anniverssary jijini Nairobi hadi eneo lililoko nje ya jiji ili kuhakikisha fedha za mlipa-ushuru zinatumika vyema, vilevile kuzuia kutatizwa kwa shughuli za tume mara kwa mara.

Chebukati aidha amependekeza kufanyika kwa mabadiliko kadhaa ikiwa njia mojawapo ya mikakati ya kupunguza visa vya utumiaji mbaya wa raslimali za umma. Kadhalika amesema watafanya uchujaji mwafaka wa wafanyakazi wa IEBC ili wanaofaa ndio wawe katika jopokazi la tume.

Kwa upande wake Kamishna Abdi Guliye amezungumzia suala la Afisa Mkuu Mtendaji Ezra Chiloba kupewa likizo ya lazima, akisema waligundua kwamba taratibu zinazofaa hazikufuatwa wakati wa ununuaji wa mali ya umma wakati wa uchaguzi ndipo wakaagiza ukaguzi kufanywa. Baada ya ripoti ya ukaguzi kubainisha kuwa sheria haikufuatwa waliamua kuchukua uamuzi huo.

Kamishna Boya Molu amesema alishangazwa na hatua ya makamishna walijiuzulu kusema kwamba walifanya hivyo kwa kuwa Chebukati alishindwa kuashiria uongozi bora akisema madai hayo hayana msingi.

Wakati uo huo ameongeza kuwa kufuatia uongozi wa Chebukati walifanikiwa kuandaa uchaguzi mkuu kwa njia huru pamoja na uchaguzi wa marudio ya uchaguzi wa urais, licha ya changamoto kadhaa zilizowakumba. Vilevile chaguzi ndogo katika maeneo mbalimbali ya nchi, mbali na kuboresha utoaji huduma na kugatua ofisi zao katika kaunti mbalimbali.