Takriban raia kumi na watatu wa kigeni wamekamatwa kwa kuwa na vibali ghushi au visivyofaa vya kazi katika oparesheni inayoendeshwa na serikali

Takriban raia kumi na watatu wa kigeni wamekamatwa kwa kuwa na vibali ghushi au visivyofaa vya kazi katika oparesheni inayoendeshwa na serikali

Takriban raia kumi na watatu wa kigeni wamekamatwa kwa kuwa na vibali ghushi au visivyofaa vya kazi katika oparesheni inayoendeshwa na serikali kuwanasa raia ambao wanahudumu nchini kinyume na sheria. Akizungumza mapema leo alipofanya kikao na Chama cha Sekta Binfasi KEPSA, Waziri wa Masuala ya Humu Nchini Fred Matiang’i amesema kwamba raia elfu mbili wamepewa stakabadhi za kazi katika shughuli ambayo itaendelea hadi mwezi Julai mwaka huu. Aidha amesema vibali ghushi vilivyonaswa vimekabidhiwa Idara ya Upelelezi CID kwa uchunguzi.

Amesema baada ya shughuli hiyo kukamilika makundi yaliyobuniwa na Inspekta Mkuu wa Polisi Joseph Boinett yatazunguka katika maeneo mbalimbali kuwanasa raia wa kigeni watakaopatikana na vibali ghushi. Aidha amesema wizara yake itabuni mswada ambao utawashinikiza watakaopatikana bila vibali vya kazi kujilipia tiketi zao za ndege za kurejea nchini mwao.

Hata hivyo amesema changamoto kuu ni kuwa baadhi ya watu wanashindwa kuzingatia taratibu zilizowekwa, badala yake kutumia njia za mkato kupata vibali hivyo. Ikumbukwe Matiang'i alitoa makataa ya siku sitini kwa raia wa kigeni wanaohudumu nchini na ambao hawana stakabadhi halali kufanya hivyo, la sivyo warejeshwe nchini mwao baada ya muda huo kukamilika. Makataa hayo yalianza tarehe 21 mwezi huu.