Masaibu yaendelea kumwandama Miguna Miguna:

Masaibu yaendelea kumwandama Miguna Miguna:
Masaibu yaendelea kumwandama Miguna Miguna: Carren Omae
Huenda mipango ya Mwanamikakati wa Muungano wa NASA Miguna Miguna, kurejea nchini isitimie hivi karibuni. Saa chache baada ya Mahakama Kuu kuamua kuwa Miguna ni raia halisi wa Kenya, serikali imefutilia mbali uamuzi huo na kusema itakata rufaa. Aidha huenda msimamo hiyo mikali ikawa mwanzo kwa kipindi kirefu cha mivutano baina ya serikali, upinzani na mahakama.
Katika barua, Wizara ya Masuala ya Ndani ya Nchi imesisitiza kuwa hatua ya kumfurusha nchini Miguna ilichukuliwa kwa mujibu wa sheria kwa kuzingatia kuwa yeye ni raia wa Canada kwani cheti chake cha usafiri cha Kenya hakikupatikana kwa njia ya kisheria.
Kadhalika, wizara hiyo kupitia Katibu wake Mkuu Karanja Kibicho, imelalamikia agizo lililotolewa leo na mahakama la kutakiwa kuwasilisha cheti hicho mahakamani katika kipindi cha siku saba. Katika barua hiyo, serikali imetaja Miguna kuwa mhalifu kwa kujihusisha na Vuguvugu la Upinzani, National Resistance Movement, NRM.
Hata hivyo, akizungumza kwa njia ya simu akiwa nchini CANADA, Miguna amemsifia Jaji Kimaru kwa kufanya uamuzi anaoutaja kuwa wa busara huku akimkosoa Kibicho.
Miguna Miguna amesisitiza kuwa ana haki ya kurejea nchini kadhalika kuapa kuwasilisha kesi dhidi ya serikali na maafisa wengine kadhaa.
Jaji  Kimaru katika uamuzi wake mapema leo, alimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Gordon Kihalagwa, kuwasilisha mahakamani paspoti ya Miguna katika kipindi cha siku saba zijazo.
Wakati uo huo, aliwapata na hatia Inspekta Mkuu wa Polisi, Jospeh Boinet na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi, DCI, George Kinoti kwa kukiuka agizo na mahakama.
Mawakili waliomwakilisha Miguna wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo wanasema uamuzi wa leo ni wa haki. James Orengo ni mmoja wa mawakili hao.
Kauli hiyo imesisitizwa na wakili na Mbunge Maalumu, Otiende Amollo ambaye anasema serikali inastahili kuheshimu maamuzi na uhuru wa idara ya mahakama.
Wiki moja iliyopita, Waziri wa Masuala ya Ndani ya Nchi, Fred Matiang'i alitoa agizo la kufurushwa nchini kwa Miguna baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na vuguvugu la NRM, vilevile kuwa miongoni mwa walioongoza hafla ya kuapishwa kwa Raila Odinga.