Ripoti kuhusu sakata ya NYS yajadiliwa

Na, Mike Nyagwoka,
Hatimaye ripoti ya Kamati ya Uhasibu wa Umma ya Bunge la Kitaifa, PAC kuhusu sakata ya zaidi ya shilingi bilioni 1 katika Taasisi ya Kitaifa ya Huduma za Vijana, NYS imeanza kujadiliwa . Ripoti hiyo iliyowasilishwa  bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Uhasibu, Nicholas Gumbo imependekeza hatua mbalimbali kuchukuliwa dhidi ya wahusika ikiwamo kuchunguzwa zaidi na kupigwa marufuku kwa aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi, Anne Waiguru kushikilia wadhfa wowote wa umma.

Aidha ripoti hiyo imependekeza kuchunguzwa kwa gavana wa Benki Kuu ya Kenya, Dkt Partrick Njoroge pamoja na maafisa  wengine kuhusu madai kwamba walichangia kufujwa kwa fedha za umma kwa kutozuia uhamisho wa mamilioni ya pesa kutoka kwenye akaunti za Wizara ya Ugatuzi hadi kampuni kadhaa zilizopewa kandarasi mbalimbali.
Kadhalika zaidi ya kampuni 100  zikiwamo kampuni tatu za  uwakili zilizokuwa na kandarasi zimeorodheshwa huku PAC ikitaka uhusiano kati ya wakurugenzi wake na maafisa wa Wizara ya Ugatuzi kuchunguzwa. Kwenye ripoti hiyo jukumu kuu limepewa Tume ya Maadili na Kukabili  Ufisadi, Idara ya Upelelezi na Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ili kuchukua hatua zifaazo.

Mbali na uchunguzi wahusika wote wametakiwa kufanyiwa  tathmini ya mali waliyomiliki  kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2012 vilevile akaunti zote za NYS. Hayo yakijiri mjadala mkali umeibuka bungeni kufuatia kuwasilishwa kwa ripoti hiyo. Mbunge wa Cherangany, Wesley Korir ni miongoni mwa waliochangia.