Bei ya unga yapunguzwa

Na, Caren Omae
Ni rasmi sasa kwamba bei ya unga wa mahindi imepungua. Kuanzia leo serikali imesambaza unga kwenye maduka ambayo inauzwa kwa shilingi 90 kwa pakiti ya kilo mbili. Radio Maisha imebainisha kuwa unga unaouzwa katika maduka mengi jijini Nairobi una nembo ya serikali jinsi alivyoahidi jana Waziri wa Kilimo Willy Bett. Aidha wateja wamepewa maagiza kutochukua zaidi ya pakiti mbili za unga, kutokana na uhaba wa bidhaa hiyo.

Hata hivyo baadhi ya maduka hayajapokea unga huo na kuendelea kuuza kwa bei ghali huku mengine yakiwa hayana unga huo.
Siku ya Jumanne, serikali ilitangaza kuwa unga utakaokuwa na nembo ya serikali utauzwa kwa shilingi 90 na kwamba itawatuma maafisa wake kukagua hali ilivyo ili kuwazuia mawakala kujinufaisha na mpango wa serikali kupunguza bei ya unga. Hatua ya kupunguzwa kwa bei hiyo imepokelewa na wananchi kwa hisia mbalimbali huku wengine wakisema hali hiyo itapunguza gharama za maisha. Aidha wengine wana maoni kwamba kupunguzwa kwa bei hiyo ni propaganda tu za serikali.

Ikumbukwe bei ya unga huo imekuwa ikiuzwa kwa kati ya shilingi 150-199 kwa pakiti ya kilo mbili kwa kipindi cha majuma kadhaa yaliyopita. Hali hiyo iliilazimu serikali kuidhinisha wafanyabiashara kununua mahindi kutoa mataifa ya nje bila kutozwa kodi hivyo kuchangia kupungua kwa bei hiyo ya mahindi.
Wiki moja iliyopita tani 30 za mahindi ziliwasili humu nchini kutoka Mexico huku tani nyingine zaidi zikitarajiwa kuwasili kwa muda wa siku chache zijazo. Serikali imesema mahindi hayo yatanunuliwa kutoka Afrika Kusini, Misri, Ethiopia na Zambia.