Raila amtetea Joho

Na Sophia Chinyezi
Licha ya Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa, Francis Nyenze kusema Chama cha Wiper kitajiondoa katika muungano wa NASA iwapo Kalonzo Musyoka hatateuliwa kupeperusha bendera ya urais, Kiongozi wa ODM, Raila Odinga amesisitiza kuwa muungano huo ungali imara.

Akizungumza baada ya kuongoza hafla ya kufungwa kwa Kongamano la Afya la Uwekezaji  katika Chuo Kikuu cha Kisii, Raila aidha ameshtumu suala la kuhangaishwa kwa Gavana wa Mombasa, Hassan Joho kuhusu stakabadhi zake za masomo, akisema serikali inahusika. Amewaeleza viongozi wa Jubilee kwamba muda wao wa kuhudumu umekamilika na kwamba wanastahili kujiandaa kuondoka uongozini.

Raila aidha amezishauri serikali za kaunti kuwalipa madaktari mishahara ya kipindi walichogoma, ikizingatiwa kwamba tayari walikuwa wametengewa fedha. Aidha ameeleza haja ya kubuniwa kwa Tume ya Huduma za Afya ili kuimarisha usimamizi utakaoboresha sekta hiyo, ukiwamo utoaji huduma hospitalini.