Wiper yatishia kuondoka NASA

Carren Omae

Chama cha Wiper kimetoa makataa ya siku tano kwa Muungano wa NASA kumtangaza atakayepeperusha bendera ya muungano huo, la si hivyo kiongozi wao Kalonzo Musyoka ajiondoe. Kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa, Francis Nyenze amesema ni sharti Kalonzo atangazwe kuwa mpeperushaji wa bendera ya muungano huo.
Amemtaka Kiongozi wa ODM, Raila Odinga kuheshimu mkataba uliotiwa saini mwaka 2013 kwamba wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu ingekuwa zamu ya Kalonzo kuwania urais.

Nyenze ambaye ni mmoja wa viongozi katika kamati maalum iliyotwikwa jukumu la kumchagua mmoja miongoni mwa viongozi wa muungano wa NASA amesema msimamo wake ni wa wanachama wengie wa Wiper.


Hayo yanajiri huku viongozi wengine wa Wiper wakisisitiza kwamba wangali katika muungano wa NASA japo wanasisitiza kuwa Kalonzo ndiye anayefaa. Wakiongozwa na Seneta wa Mombasa, Omar Hassan viongozi hao sasa wanawataka Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, Moses Wtangula na Musalia Mudavadi kufanya mazungumzo na kuafikiana kuhusu suala hilo.