Joho asisitiza Serikali inamwandama

Mike Nyagwoka

'Sitababaishwa kamwe na serikali.' Ndiyo kauli aliyoirejelea Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho baada ya kurekodi taarifa katika Idara ya Upelelezi, DCI Mombasa. Akiwahutubia wanahabari akiwa amezingirwa na viongozi kadhaa na wafuasi wake, Joho ameweka bayana kuwa masaibu yake yametokana na tofauti baina yake na Rais Kenyatta.


Hatimaye baada ya vuta nkuvute baina ya serikali na Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho kuhusu madai kwamba cheti chake cha KCSE si halali, gavana huyo amerekodi taarifa huku akisisitiza kuwa hana hatia. Joho aliandamana na viongozi kadhaa wa eneo la Pwani mbali na mawakili waliongozwa na Seneta wa Siaya, James Orengo.
Awali mvutano ulishuhudiwa kati ya wafuasi wake na maafisa wa polisi waliojaribu kuwazuia kuingia katika ofisi za makao makuu ya idara hiyo.


Wanahabari vilevile walizuiwa kuingia katika ofisi hizo huku barabara zote zinazoelekea eneo hilo zikifungwa.
Baada ya kuhojiwa,  Joho amesisitiza kuwa licha ya kuandamwa na idara mbalimbali za serikali hababaishwi na masaibu yanayomkumba. Vilevile amerejelea kauli ya Rais dhidi yake alipozuru Kaunti ya Mombasa huku akisema huenda masaibu yanayomkumba yanatokana na kauli hiyo. Amesema licha ya mawimbi yote haya, jina lake litakuwa katika debe Agosti 8.


Uchunguzi wa madai dhidi yake utaendelea huku watu zaidi wakitarajiwa kuhojiwa.