Rais wa Somalia kuzuru Kenya

Na Suleiman Yeri
NAIROBI, KENYA,

Sheria kali za Kenya kuhusu safari za ndege kutoka Somalia, udhibiti wa anga na hatma ya Jeshi la Kenya, KDF nchini Somalia ni miongoni mwa masuala makuu yatakayojadiliwa wakati wa ziara ya kwanza ya Rais wa taifa hilo, Muhamed Farmajo humu nchini Alhamisi wiki hii.


Hapo jana, Msemaji wa Ikulu Manoah Esipisu alidokeza kuwa masuala ya uhamiaji, ushirikiano wa safari za ndege na usalama wa ukanda huu ni miongoni mwa mambo makuu yatakayojadiliwa wakati wa mkutano huo.


Farmajo aliyeshinda kiti hicho mwezi mmoja uliopita anatarajiwa kuendelea kushinikiza ombi la kutaka ndege kutoka Somalia kutua humu nchini mara mbili kwa siku suala ambalo limekuwa likijadiliwa kuanzia mwaka 2015.