Wanajeshi watumwa Baringo, Elgeyo Marakwet, Pokot Magharibi na Laikipia kuimarisha hali

Wanajeshi watumwa Baringo, Elgeyo Marakwet, Pokot Magharibi na Laikipia kuimarisha hali

Na Sophia Chinyezi

Siku mbili tu baada ya kutangaza kuwa serikali yake imejitolea kuwalinda wananchi na mali zao kwa mujibu wa katiba, Rais Uhuru Kenyatta ameamuru kutumwa kwa wanajeshi wa KDF kwenye Kaunti za Baringo, Elgeyo Marakwet, Pokot Magharibi na Laikipia kuimarisha usalama. Rais amesema Baraza la Kitaifa la Usalama ambalo analiongoza, limeidhinisha kupelekwa mara moja kwa wanajeshi hao ili kuwasaidia polisi wa kawaida kurejesha amani kwenye maeneo hayo. 

Ameyasema hayo katika Chuo cha Mafunzo ya Polisi wa Utawala eneo la Embakasi Nairobi, alipoongoza hafla ya kufuzu kwa makurutu elfu tatu, mia tisa themanini na watano ambao wamekamilisha mafunzo ya miezi tisa. Rais Kenyatta amesema waliokaidi agizo la kusalimisha silaha wanazozimiliki kinyume na sheria ni maadui wa taifa hili na kwamba watakabiliwa vilivyo.

Ameongeza uamuzi wa kuwapelekea wanajeshi kwenye kaunti hizo umetokana na kukithiri kwa utovu wa usalama. Amesema serikali imewekeza zaidi katika kuwapa maafisa wa usalama vifaa vya kisasa na vya kutosha kama vile magari na helikopta kusaidia katika oparehseni.

Ikumbukwe katika hotuba yake Jumatano wiki hii bungeni, Rais aliwataja wanasiasa kuwa wachochezi wa mauaji, wizi wa mifugo na wakazi kukoseshwa makao.