Sonko na wenzake wawasilisha stakabadhi zao kwa Jubilee

Sonko na wenzake wawasilisha stakabadhi zao kwa Jubilee

Na Carren Omae

Kinyang'anyiro cha kiti cha ugavana Kaunti ya Nairobi kwa tiketi ya Chama cha Jubilee kinaendelea kushika kasi. Siku mbili baada ya aliyekuwa mgombea urais, Peter Keneth kuwasilisha stakabadhi zake, wanasiasa wanaokimezea mate kiti hicho vilevile wamewasilisha stakabadhi zao za uteuzi katika makao makuu ya Jubilee.

Wanasiasa hao wanaojumuisha kundi kwa jina, Team Nairobi, akiwamo Seneta Mike Sonko, Askofu Magret Wanjiru na Mbunge wa Dagoretti Kusini Dennis Waweru, wamesema wana imani kwamba Jubilee ndiyo itakayoibuka na ushindi wakati wa uchaguzi wa Agosti 8. Wamesisitiza kuendeleza ushirikiano bila mgawanyiko kushuhudiwa. Johnson Sakaja, anakilenga kiti cha useneta.

Sonko kwa upande wake ametumia fursa hiyo kufutilia mbali madai kwamba vyeti vyake vya elimu si halali.

Wakati uo huo, Mkuu wa Jopo-kazi la uchaguzi katika Jubilee, Raphael Tuju amewahakikishia kwamba uteuzi wa chama hicho utakuwa huru na wa haki.

Hapo jana, Sonko alilalamikia kunyimwa cheti cha maadili na hivyo kudai kuwapo kwa njama ya kumnyima tiketi ya Jubilee kuwania ugavana, Kaunti ya Nairobi.