Madaktari wa hospitali ya Kenyatta wangali wanagoma

Madaktari wa hospitali ya Kenyatta wangali wanagoma

Na, Beatrice Maganga

Ni madaktari wa Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, KNH pekee kote nchini ndio hawajasitisha mgomo, huku mkataba wa kurejea kazini kwa madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Moi Eldoret ukisainiwa leo hii.  

Muungano wa Madaktari, KMPDU umeushtumu usimamizi wa KNH kwa kuchelewesha utaratibu wa kuhakikisha madaktari wa hospitali hiyo wanarejea kazini. Katibu Mkuu wa muungano huo, Ouma Oluga amesema madaktari hao wana mkataba tofauti na serikali, hivyo ni lazima matakwa yao yatimizwe kabla ya kurejea kazini.

Akizungumza katika hoteli moja mjini Naivasha alipoongoza utiaji saini mkataba wa kurejea kazini kwa madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Moi Eldoret, Oluga aidha ameishtumu hospitali ya KNH kwa kuwasimamisha kazi baadhi ya madaktari waliokuwa wakigoma. Kauli yake imetiliwa mkazo na Mwenyekiti wa KMPDU, Samuel Oroko.

Madaktari wa KNH wamekataa kurejea kazini hadi wasimamizi wa hospitali hiyo watakapowarejesha kazini wenzao kumi na wawili walioasimamishwa kazi. Afisa Mkuu Mtendaji wa hospitali hiyo, Lily Koros alitangaza kufutwa kwao licha ya kuonywa dhidi ya kushiriki mgomo ulioharamishwa na mahakama.

Mapema wiki hii, pande zilizokuwa zikishiriki mazungumzo ya kutafuta suluhu kuhusu matakwa ya madaktari zilitangaza kusitishwa kwa mgomo huo uliodumu kwa siku 100.