Masaibu ya Waiguru yangalipo

Na, Beatrice Maganga/ Sophia Chinyezi

Huenda masaibu yanayomkomba aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi, Anne Waiguru yasifikie kikomo hivi karibuni. Kamati ya Bunge ya Uhasimu, PAC imependekeza kwamba hali yake ya kimaisha ichunguzwe kufuatia tuhuma za ufisadi dhidi yake kuhusiana na  Taasisi ya Kitaifa ya Huduma za Vijana, NYS.

Lengo la uchunguzi huo ni kubaini iwapo hali yake ya kimaisha inaendana na mshahara aliokuwa akipokea au la. PAC vilevile imependekeza kushtakiwa kwa Seneta wa Elgeyo Marakwet, Kipchumba Murkomen na washukiwa wengine kufuatia sakata hiyo.

Wabunge hao pia wanataka Gavana wa Benki Kuu, Patrick Njoroge achunguzwe. Katika ripoti iliyowasilishwa bungeni leo adhuhuri, PAC imependekeza Waiguru azuiliwe kushikilia ofisi yoyote ya umma iwapo atapatikana na hatia, kufuatia tuhuma zilitokana na utendakazi wake alipokuwa katika Wizara ya Ugatuzi. Vilevile kwa sababu ya kukikuka Sehemu ya Sita ya Katiba.

Muda mfupi baada ya uamuzi huo, Seneta Murkomen aliwahutubia wanahabari na kulikosoa vikali pendekezo la PAC kwamba ashtakiwe kwa kuhusishwa na sakata ya NYS. Murkomen ameishtumu kamati hiyo inayoongozwa na Nicholus Gumbo kwa madai ya kufanya uchunguzi duni kuhusu sakata hiyo huku akidai kuwa ametajwa kwa vile alikataa kuwahonga wanakamati wa PAC ili wampendelee katika uchunguzi wao.

Aidha ameshanganzwa na pendekezo la kamati hiyo kwamba kampuni yake ya uanasheria ishtakiwe kwa kuhusika ubadilishanaji wa fedha kwa njia ya ulaghai ilhali haijatoa ushahidi wa kuihusisha kampuni hiyo na kitendo hicho.