Kalonzo ajitayarisha kwa kinyang'anyiro cha urais

Kalonzo ajitayarisha kwa kinyang'anyiro cha urais


Na, Beatrice Maganga

Kinara wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka kwa mara nyingine amepinga madai kwamba huenda akajitenga na Muungano wa NASA iwapo hatateuliwa kupeperusha bendera ya urais katika muungano huo. Akizungumza alipowasilisha mbele ya chama chake karatasi za uteuzi kukiwania kiti hicho katika makao makuu ya Wiper jijini Nairobi, Kalonzo amesema uteuzi wa leo ni dhihirisho kwamba yu tayari kwa kinyang'anyiro cha urais.

Ikumbukwe viongozi wote wa NASA ambao ni Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula wanalenga kuipeperusha bendera ya urais ya muungano huo.

Siku chache zilizopita, utafiti wa Infortack ulibainisha kwamba asilimia 68.3 ya wafuasi wengi wa NASA wanampendelea Raila Odinga apeperushe bendera ya muungano huo, Kalonzo asilimia 13.1, Mudavadi asilimia 12.3 na Wetangula asilimia 2.2 pekee. Kalonzo la Wetangula walipinga vikali matokeo hayo wakidai yalichochewa kupitia rushwa. NASA inapanga kumtangaza mgombea wake wa urais mapema mwezi ujao.