Mhasibu Mkuu wa serikali asema hatabanduka ofisini

Mhasibu Mkuu wa serikali asema hatabanduka ofisini

Na Carren Omae

Huku bunge la Kitaifa likisubiria kuona iwapo litatii agizo la mahakama la kulizuia kuendela kujadili ombi la kumtaka Mhasibu Mkuu wa Serikali, Edward Ouko kuondolewa ofisini huenda mjadala kuhusu suala hilo ukachukua mkondo mwingine, kufuatia madai kwamba Kamati ya Fedha Bungeni ina njama ya kumwondoa ofisini.

Madai hayo yamerejelewa leo na Ouko huku akilalamikia jinsi utaratibu wa kushughulikia ombi hilo unavyoendeshwa.
Jinsi ilivyo miongoni mwa maafisa wa serikali wanaohusishwa na sakata mbalimbali, hali kumhusu Mhasibu Mkuu wa Serikali Edward Ouko haijakuwa tofauti. Ouko amekuwa mwepesi wa kuapa kutoondoka ofisini akisema hakuna uchunguzi unaoendelea dhidi yake.

Katika kikao na wanahabari Ouko amesema amewaagiza mawakili wake kuwasilisha kesi dhidi ya Wakili Emanuel Mwagambo aliyewasilisha ombi la kutaka aondolewe ofisini akisema amemharibia sifa.
Amesisitiza kwamba hatua yake ya kuwasilisha kesi mahakamani kulizuia bunge kujadili ombi hilo, ni ya kuhakikisha kuwa uchunguzi dhidi yake unafanywa kwa njia ya haki. Otiende Omollo ni wakili wake.

Wakati uo huo, amekana madai yote dhidi yake, ukiwamo ufujaji wa fedha katika ofisi yake, ukiukaji wa katiba kwa kutowasilisha ripoti kwa wakati, ukiukaji wa sheria za ununuzi miongoni mwa madai mengine.

Ikumbukwe Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi EACC ilipendekeza Ouko kushtakiwa dhidi ya tuhuma hizo ila, zikaondolewa na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma.
Jumanne wiki Ijayo Spika Justin Muturi anatarajiwa kutoa uamuzi iwapoa Bunge litaendelea kulijadili suala hilo au la.