Upinzani waahidi kushirikiana

Na Carren Omae
''Tutashirikiana kwa lengo la kuing'atua Jubilee madarakani,''  wameapa viongozi wa upinzani, Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula wakati wa mkutano uliofanyika leo katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi. Ajenda kuu ya mkutano huo imekuwa kudhihirisha umoja miongoni mwa vigogo hao ambao tayari wametangaza nia ya kuwania urais wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti nane.
Zaidi ya wajumbe elfu nne wa vyama vya ODM, Wiper, Ford Kenya ANC, na kile cha KANU waliwasili katika mkutano huo, huku kilele kikikuwa ni kutiwa saini kwa makubaliano ya kusalia pamoja kwa viongozi wa vyama, kufanya kampeni pamoja na kubainisha ni nani hasa watakayemuunga mkono kupeperusha bendera kuwania kiti cha urais wakati wa uchaguzi mkuu ujao. James Orengo ni Seneta wa Siaya.
Vigogo hao wamesisitiza umuhimu wa kuhakikisha makubaliano ya leo yanatekelezwa. Musalia Mudavadi ni Kiongozi wa Chama cha Amani National Congress, na mwasisi wa wazo la kuubuni muungano wa NASA.
Akiishtumu serikali ya Jubilee, Kinara wa CORD Raila Odinga, amesema licha ya kutoyakubali mageuzi yaliyofanyiwa sheria za uchaguzi hawatashiriki maandamano katika kipindi cha siku 30 zijazo. Aidha amesema watahakikisha uchaguzi mkuu ujao unaandaliwa kwa njia ya huru na haki ili kufanikisha ajenda yao ya kuiondoa Jubilee mamlakani.
Kalonzo kwa upande wake amebadili msimamo wa awali akisame yu tayari kumuunga mkono atakayeteuliwa kupeperusha bendera ya NASA, lengo likiwa kuondoa Jubilee mamlakani.
Wamewashtumu viongozi wa Jubilee kutokana na kukithiri kwa ufisadi.
Huku ikisubiriwa kuona ni nani atakayeipeperusha bendera ya NASA, lililokuwa kuu kutoka kwao, ni mwito wa kuungana na kusalia imara.