Mchujo wa maafisa wapya walioteuliwa kujiunga na IEBC wakamilika

Mchujo wa maafisa wapya walioteuliwa kujiunga na IEBC wakamilika

Na Beatrice Maganga
Bunge la Kitaifa, linasubiriwa kuyajadili majina ya walioteuliwa kwa nyadhifa za makamishna wa Tume ya Uchaguzi, IEBC baada ya kukamilika kwa mchujo uliokuwa ukiongozwa na Kamati ya Haki na Sheria ya Bunge la Kitaifa. Kamati hiyo leo hii imewahoji Profesa Abdi Guliye, Margaret Wachanya na Paul Kurgat.
Wa kwanza kufika mbele ya kamati hiyo iliyo chini ya uenyekiti wa Mbunge wa Ainabkoi, Samuel Chepkonga amekuwa Balozi Paul Kurgat. Kurgat ametumia fursa hiyo kutoa changamoto kwa kamati hiyo kufanikisha mswada wa kuhakikisha walio na changamoto za maumbile wanapata fursa ya kupiga kura wakati wa uchaguzi mkuu ujao.Kwa upande wake, Margaret Wachanya amesema atazingatia maadili ya utendakazi na hatakubali ushawishi wa aina yoyote kuathiri utendakazi wa tume hiyo. Profesa Abdi Guliye amekuwa wa mwisho kuhojiwa huku akitakiwa kueleza iwapo anaanini uteuzi wa makamishna wa IEBC ulifanywa kwa kuzingatia usawa wa kikabila.
Waliohojiwa Jana ni Mwenyekiti Mteule, Wafula Chebukati, Roseylne Akombe na Boya Molu.
Kamati hiyo ya uchujaji leo alasiri imeendeleza kikao cha kukamilisha maandalizi ya ripoti hiyo ya mchujo ambayo itawasilishwa bungeni Jumanne wiki ijayo na kujadiliwa katika kikao maalumu kilichoitishwa na Spika wa Bunge la Kitaifa, Justine Muturi. Mwenyekiti wa kamati hiyo, Samuel Chepkonga ameeleza matarajio kwamba bunge litayaidhinisha majina hayo ili kuwe na makamishna wapya wa kusimamia usajili wa wapiga-kura utakaoanza tarehe kumi na sita mwezi huu.
Jina la Mwenyekiti Mteule wa Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi EACC, Askofu mstaafu, Eliud Wabukhala vilevile litawasilishwa bungeni kwa mchujo.