Mark Too azikwa
Na, Beatrice Maganga
Hatimaye aliyekuwa Mbunge Maalumu, Marehemu Mark Too amezikwa nyumbani kwake Maziwa Farm, Kaunti ya Uasin Gishu. Akihutubu wakati wa halfa hiyo, Rais Uhuru Kenyatta amemtaja Marehemu kuwa kiongozi aliyekuwa mpatanishi mkuu na mpenda amani. Rais Kenyatta ametoa wito kwa wananchi kuiga mfano wa Too wa kuhubiri amani nchini.
Rais aidha amemtaja Too kuwa kiongozi aliyempa usaidizi mkubwa katika harakati zake za kisiasa na hata kuwa Rais wa taifa hili.
Naibu wa Rais, William Ruto kwa upande wake amemtaja Too kuwa kiongozi aliyekuwa na misimamo mikali na malengo makuu maishani. Ruto aidha amemtaja Too kuwa kiongozi aliyetangamana na watu wa matabaka mbalimbali na kuwasadia kufanikisha malengo yao maishani.
Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Adan Duale ametumia hafla hiyo ya mazishi kumsuta Kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka kwa kutishia kumshtaki katika Mahakama ya ICC kwa madai ya kuwachochea wenyeji wa Garissa dhidi ya jamii ya Akamba inayoishi eneo la Garissa. Duale amesisitiza kwamba sauti iliyonaswa na kudaiwa kuwa yake, ni njama ya watu fulani wanaolenga kumharibia sifa.
Awali kabla ya mazishi ya Too, mwanamke aliyejaribu kupinga mazishi ya Too kwa jina Fatuma Ramadhan alilazwa hospitalini baada ya kuzirai katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta, alipokuwa akielekea kwa mazishi hayo mjini Eldoret. 
Ikumbukwe aliwasilisha kesi kupinga mazishi hayo kwa misingi kwamba mwanawe ambaye anadai kuwa Too ndiye babaye, hakuhusishwa katika mipango ya mazishi. Hata hivyo aliiondoa kesi hiyo baada ya kuahidiwa kuhusishwa katika maandalizi hayo.
Mazishi ya Too yamefanyika leo baada ya Mahakama ya Eldoret kutupilia mbali agizo lake la awali la kuyasitisha. Japo hakutoa sababu za kusitishwa kwa agizo la awali, Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Eldoret, Nicodemus Moseti ameagiza waliotajwa katika rufaa iliyowasilishwa na wakili Simon Lilan kufika mahakamani tarehe 12 mwezi huu.