CORD yasitisha maandamano

Na Carren Omae
Maandamano yaliyopangiwa kufanyika tarehe 4, Januari na muungano wa CORD kupinga mageuzi katika sheria za uchaguzi yaliyoidhinishwa na bunge, yamesitishwa. CORD imesitisha maandamano hayo kusubiri uamuzi wa kamati ya Seneti inayokusanya maoni kabla ya kuwasilisha ripoti yake katika Seneti wiki ijayo.
Vinara wa CORD Moses Wetangula na Kalonzo Musyoka, wamesema watasubiri ripoti hiyo kabla ya kutangaza hatua watakazozichukua.
Hayo yanajiri huku, Kamati ya Sheria na Haki katika Seneti iliyotwikwa jukumu la kukusanya maoni hayo, ikiendelea na vikao vyake leo hii. Waziri wa Teknolojia, Joe Mucheru ambaye amefika mbele ya kamati hiyo mapema leo ameelezea changamoto nyingi kuhusu utumiaji wa teknolojia huku akisema, akiunga mkono kuwapo kwa njia ya zamani katika shughuli ya upigaji kura.
Kamati hiyo vilevile imewahoji maafisa wa Tume ya Uchaguzi IEBC pamoja na wawakilishi wa watu wanaoishi na ulemavu katika kikao cha leo.