Wito watolewa kwa Rais Kenyatta kutoyaidhinisha mageuzi ya uchaguzi

Wito watolewa kwa Rais Kenyatta kutoyaidhinisha mageuzi ya uchaguzi

Na Beatrice Maganga

NAIROBI, KENYA, Wito umetolewa kwa Rais Uhuru Kenyatta kutoyaidhinisha mageuzi yaliyofanyiwa sheria za uchaguzi Alhamisi.Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini badala yake wamemsihi Rais kuruhusu kufanyika majadiliano baina ya serikali na mrengo wa CORD ili kusuluhisha tofauti zilizopo. Maaskofu hao wamewaonya wanasiasa dhidi ya kuibua taharuki nchini ikiwa imesalia miezi saba kabla ya uchaguzi mkuu.

Wito sawa na huo umetolewa na Tume ya Uchaguzi IEBC ambayo imewasihi  wanasiasa kusitisha malumbano na kuruhusu uchaguzi mkuu ujao kuandaliwa kwa amani.Katika taarifa, IEBC imesema kuwa mabadiliko yaliyopendekezwa na tume hiyo kupitia Kamati ya Haki na Sheria yalikuwa yameidhinishwa na wabunge wa mrengo wa CORD na Jubilee na haielewi ni kwanini tofauti ziliibuka wakati wa kuidhinisha mabadiliko hayo bungeni.

Wito huo wa IEBC na maaskofu umejiri wakati ambapo serikali na upinzani zimeonesha misimamo mikali na kuchangia kupitishwa kwa mageuzi hayo yaliyoungwa mkono na wabunge wa Jubilee pekee huku CORD ikiitisha maandamano kuanzia Januari nne mwaka ujao kulalamikia hatua hiyo.

Vinara wa CORD Raila Odinga, Kalonzo Musyoka na Moses Wetangula kwa mara nyingine wamedai kwamba Jubilee inanuia kufanikisha wizi wa kura kwa kuidhinisha kutumiwa kwa mfumo wa zamani wa kupiga kura iwapo ule wa kielektroniki utakumbwa na hitilafu.