Mjadala mkali unatarajiwa leo bungeni

Na Mike Nyagwoka

mjadala mkali unatarajiwa leo bungeni

NAIROBI, Mjadala mwingine mkali unatarajiwa bungeni Alhamisi wakati wabunge watakapojadili mageuzi kwenye sheria za uchaguzi.
Hali hii inafutia misimamo mikali ambayo imechukuliwa na mirengo ya CORD na Jubilee huku CORD ikiapa kupinga mageuzi hayo na Jubilee kusisitiza lazima yatapitishwa.
Jana miungano yote miwili ilifanya mikutano ya wabunge wao suala kuu likiwa jinsi ya kufanikisha ajenda zao zinazokinzana.
Kinara wa FORD-Kenya Moses Wetangula amesisitiza kuwa iwapo kuna jambo lolote la kujadiliwa kuhusu sheria za uchaguzi linapaswa kufanywa na kamati ya pamoja iliyojukumiwa kutatua utata wa IEBC chini ya uenyekiti wa maseneta James Orengo na Kiraitu Murungi la sivyo warejee kwa maandamano.
Akizungumza kwenye hafla nyingine, Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria amekariri kuwa lazima mageuzi hayo yapitishwe. Kwa mujibu wa Kuria, shinikizo lao linatokana na uhalisia wa mambo kuhusu uwezekano wa vifaa vya eletroniki kufeli.