SRC kuzindua muongozo mpya wa malipo ya wafanyakazi

SRC kuzindua muongozo mpya wa malipo ya wafanyakazi

Na Beatrice Maganga

Tume ya Kuratibu Mishahara ya Wafanyakazi wa Umma SRC inazindua muongozo mpya wa malipo kwa wafanyakazi wa umma.
Muongozo huo unazinduliwa baada ya tume hiyo kukamilisha tathmini ya sekta zote za umma kubainisha kiwango kinachostahili kulipwa wafanyakazi wa sekta hizo. Ina maana kwamba mishahara ya wafanyazi wanaolipwa juu zaidi itasalia jinsi ilivyo kwa sasa huku wengine wakiongezewa kwa lengo la kuisawazisha mishahara hiyo.
Kulingana na Mwenyekiti wa SRC Sarah Serem, kunazo sekta zilizowekewa mishahara ya juu zaidi kinyume na inavyostahili na muongozo mpya unalenga kuhakikisha usawa wa malipo na kazi inayofanywa. Miongoni mwa wanaotarajiwa kunufaika kupitia kwa muongozo huo ni madaktari na wahandishi.  
katika mpango huo mpya utakaoanza mwaka ujao mwezi wa Julai wafanyakazi wa umma watawekwa katika makundi ya Gredi A ambayo ni ya chini zaidi hadi E ambayo ni ya juu. Aidha makundi hayo yatakuwa na mengine chini yake ya A1, A2, A3 na mengine.
Serikali imekuwa ikilalamikia gharama ya juu inayotokana na kuwalipa mishahara ya wafanyaki wa umma. Kwa sasa kima cha shilingi bilioni 627 kimekuwa kikitumika kulipa mishahara ya wafanyakazi takriban laki saba wa sekta ya umma.
Serem hata hivyo amesema hakuna mipango ya kuwafuta wafanyakazi wengine japo watakaoajiriwa baada ya muongozo huo watalipwa kwa kuzingatiwa viwango vipya vya mishahara.