Mailu na Muraguri wahojiwa tena na wabunge

Na Suleiman Yeri/Carren Omae

Waziri wa Afya Dkt. Cleophas Mailu na Katibu wake, Dkt. Nicholas Muraguri wameomba Kamati ya Afya ya Bunge la Kitaifa kuwapa muda zaidi ili kubainisha kiwango cha fedha kitakachotumika kuweka kliniki tamba ambazo zingali katika bohari mjini, Mombasa.
Wawili hao walikosa kuieleza kamati hiyo kiwango kinachohitajika kuweka kliniki hizo, baada ya Mbunge wa Tongeren Dkt. Eseli Simiyu kutaka kujua gharama ya kliniki hizo mia moja ambazo zote zimegharimu shilingi bilioni moja.
Wakati uo huo, Mailu ameoneka kumlaumu Mhasibu Mkuu katika wizara, Bernard Muchere kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kabla ya kupata majibu kutoka kwa wahusika katika wizara hiyo kuhusu madai ya kupotea shilingi bilioni 5.
Vilevile wanachama wa kamati hiyo wametaka kufahamu ni kwa nini wizara ingali inazitengea fedha baadi ya hospitali ikizingatiwa kuwa sekta hiyo iligatuliwa. Hata hivyo Mailu amejitetea kuwa hospitali zinazopokea fedha hizo ni zile ambazo zilikuwa za mikoa kwa sababu bado zinawahudumia wagonjwa kama awali.